Katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko hususan kipindupindu, Kitengo cha usimamizi wa taka na usafi kimefanya ziara ya kutoa elimu ya usafi kwa wafanyabiashara katika Soko la Ilungu Kata ya Nyigogo Wilayani Magu , ikiwa ni sehemu ya jitihada za kulinda afya za wananchi hasa katika msimu huu wa mvua na kipindi cha msimu wa matunda aina ya maembe.

Akizungumza na wafanyabiashara hao leo Ijumaa Desemba 19 , Mkuu wa Kitengo hicho Bwa. Francisco Ndazi alisisitiza umuhimu wa kudumisha usafi wa mazingira ya soko, akiwataka wafanyabiashara wote kuzingatia utaratibu uliowekwa wa kufanya usafi kila siku ya Ijumaa kwa kushiriki kikamilifu bila kukosa.
Aidha, aliwataka kuacha tabia ya kutupa taka ovyo ndani ya soko, na badala yake kutumia eneo maalum lililotengwa kwa ajili ya kumwagia taka ili kusaidia kulinda afya ya jamii na mazingira.

Mkuu huyo alibainisha kuwa ziara kama hiyo itaendelea kufanyika katika masoko yote ya halmashauri ili kuhakikisha elimu ya usafi inawafikia watu wote, huku akitoa wito kwa wananchi wote kuzingatia usafi wa mazingira kipindi chote cha mvua.
Kwa upande wao, wafanyabiashara wa soko hilo walipongeza ziara hiyo, wakieleza kuwa imetolewa kwa wakati muafaka na kuahidi kuzingatia usafi wa mazingira kwa manufaa ya wote.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa