ZAIDI ya wakazi 32,000 wa kata za Lutale na Nyanguge wilayani Magu wanatarajiwa kufaidika na mradi wa ujenzi wa wodi ya wazazi pamoja na jengo la upasuaji, miradi inayotajwa kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi wilayani humo.

Miradi hiyo yenye thamani ya Sh milioni 500 inatekelezwa katika Zahanati ya Lutale pamoja na Kituo cha Afya Nyanguge.
Hayo yamebainishwa jana Jumanne katika ziara ya Kamati Fedha, Uongozi na Mipango iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Edward Kihamba kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akiwasilisha tarifa ya utekelezaji wa mradi wa wodi ya wazazi na jengo la upasuaji katika zahanati ya Lutale kwa wajumbe wa kamati hiyo, Mganga Mfawidhi wa Kituo, Christopher Mhando amesema mradi huo uliotengewa kiasi cha Sh milioni 250, hadi sasa umefikia asilimia 60 na unatarajiwa kukamilika Machi mwaka huu.

“Mradi utakapokamilika unatarajiwa kutoa huduma kwa wakazi wapatao 16,511 wa kata ya Lutale pia wakazi wa kata jirani za Kongolo na Bujashi.
Kwa upande wa Kituo cha afya Nyanguge, wajumbe walielezwa kuwa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 80 na hadi sasa umetumia kiasi cha Sh milioni 200 kati ya milioni 250 zilizotengwa.
Wajumbe wa kamati hiyo, walieleza kuridhishwa na utekelezwaji wa miradi hiyo ambayo pamoja na mambo mengine, itapunguza adha ya gharama na kutembea umbali mrefu kufuata huduma.

Mbali na miradi hiyo, wajumbe hao pia walikagua miradi ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu 12 ya vyoo katika shule ya msingi Muungano iliyopo kata ya Kisesa, ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Itandula kata ya Lutale, ujenzi wa shule mpya ya msingi eneo la Bugumangala kata ya Nyanguge.
Pia walikagua mradi wa ujenzi wa stendi mpya ya Ilungu iliyopo kata ya Nyigogo ambao pamoja na mambo mengine wajumbe hao wakisisitiza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo ili wananchi wapate huduma kwa urahisi.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa