Na GCU - Magu
Leo Jumatatu Januari 26, 2026 Halmashauri ya Wilaya ya Magu imeanza rasmi utekelezaji wa bima ya afya kwa wote ambapo timu ya wataalamu wa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Mwanza ilitoa elimu kuhusu utekelezaji wa mkakati huo katika kikao cha kamati ya ushauri ya Wilaya (DCC) kilichoongozwa na mkuu wa wilaya ya Magu Mh. Jubilate Lawuo.
Akizungumza wakati akiwasilisha mada katika kikao hicho Afisa wanachama wa NHIF Mwanza, Mbwalila Ng'amilo amesema utekelezaji wa bima ya afya kwa wote awamu ya kwanza utahusisha kundi la wanachama wasio na uwezo ( wazee, watoto, wajawazito na walemavu) ambao watagharamiwa na serikali kwa kulipiwa kitita cha huduma muhimu kitakachotolewa na skimu za bima ya afya kwa gaharama ya shilingi 150,000 kwa kaya ya watu wasiozidi 6.

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Magu, Mh. Jubilate Lawuo alitoa wito kwa wajumbe waliopatiwa elimu ya utekelezaji wa bima ya afya kwa wote kuwa mabalozi wazuri wa kutoa elimu kwa wengine juu ya umuhimu wa bima ya afya kwa wote.
Magu imeanza utekelezaji huo baada ya serikali kupitia wizara ya afya kuzindua bima ya afya kwa wote Januari 23, 2026 jijini Dodoma ambapo Waziri wa afya Mh. Mohamed Mchengerwa alitangaza kuwa utekelezaji wake unaanza leo Januari 26/2026.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa