Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Magu wamepatiwa mafunzo maalum kuhusu utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, kufuatia serikali kutangaza rasmi kuanza kwa utekelezaji wa sheria hiyo nchini Januari 26, 2026.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo madiwani ili waweze kuelewa majukumu yao katika kusimamia na kuhamasisha utekelezaji wa bima hiyo katika maeneo yao.

Mafunzo hayo yametolewa na Afisa Wanachama wa NHIF Mwanza Mbwalila Ng’amilo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichokutana kujadili rasimu ya bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Katika maelezo yake, Ng’amilo alieleza kuwa Bima ya Afya kwa Wote inalenga kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya bila vikwazo vya kifedha.
Aidha, madiwani walisisitizwa kuwa mabalozi muhimu wa utoaji elimu kwa wananchi katika kata zao, kwa kuwahamasisha kujiunga na bima ya afya ili kuongeza uelewa na ushiriki wa wananchi katika mpango huo wa kitaifa. Walihimizwa kutumia mikutano ya hadhara na majukwaa mbalimbali kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Kwa upande wao, madiwani walieleza utayari wao wa kushirikiana na wataalamu wa afya na viongozi wa mitaa kuhakikisha utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote unafanikiwa, huku wakiahidi kusimamia kikamilifu zoezi hilo kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya sekta ya afya.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa