Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mheshimiwa Dkt. Stergomena Lawrence Tax, tarehe 24 Oktoba 2025, amekabidhi madawati 80 ikiwa ni kutimiza ahadi yake aliyowahi kuitoa kwa Shule ya Msingi Nyambitilwa, Wilaya Magu mkoani Mwanza. Katika makabidhiano hayo, Mhe. Dkt. Tax aliambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Magu, Bw. Mohamed Ramadhan.
Akizungumza na Uongozi wa shule pamoja na hadhira ya Wanafunzi wa Shule ya Nyambitilwa, Mhe Dkt. Tax amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili kufikia ndoto zao na matarajio ya wazazi wao na Taifa kwa ujumla.
Aidha, Waziri Tax ametoa wito kwa jamii na wadau wengine ikiwemo wana Magu kujenga utaratibu wa kurudisha kwa jamii kwa kutoa misaada hasa katika Sekta ya elimu ili kukabiliana na uhaba wa vifaa na miundombinu ya elimu mashuleni ikiwa ni pamoja na Wilayani Magu.
Kabla ya kuhitimisha tukio hilo la kukabidhi madawati hayo, Dkt Tax ametumia fursa hiyo kutoa rai na kuwataka Walimu na Wanafunzi waliotimiza umri wa miaka 18 na wenye Sifa za kupiga kura, kujitokeza kwa wingi kupiga Kura siku ya Uchaguzi Mkuu tarehe 29 Oktoba 2025, ili kutimiza haki yao ya Kikatiba ya kuchagua Viongozi katika ngazi ya Rais, Ubunge na Udiwani
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa