Wakati zoezi la kuripoti wanafunzi wa kidato cha tano kwa mhula mpya wa masomo 2023 likiendelea wazazi wamehimizwa kuwapeleka watoto shule ili waanze masomo kwa wakati kwakua walimu wapo tayari kufundisha na Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kuhakikisha madarasa ya kutosha yanajengwa kila shule.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Magu Rachel Kassanda wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya kuripoti kwa Wanafunzi wa kidato cha tano wa Shule ya sekondari Magu ambayo hadi sasa imepokea wanafunzi 60 kati ya wanafunzi 152 waliopangiwa kujiunga na Shule hiyo inayopatikana katika kata ya Isandula Wilayani Magu Mkoani Mwanza.
Akizungumza na Wanafunzi wa Shule hiyo DC Kassanda amesema kuwa ni vyema wanafunzi wote wakaanza masomo kwa pamoja ili asiachwe mtu nyuma na kusisitiza kuwa wazazi wa wanafunzi ambao hawajaripoti shule kuongeza juhudi ili kuhakikisha wanafunzi wote wanaripoti shule kwa wakati.
"Niwaombe wazazi waongeze juhudi ili wanafunzi waripoti shule kwani hadi sasa katika shule ya sekondari Magu idadi ya wanafunzi waliofika haifiki hata nusu ya idadi ya jumla ya wanafunzi wote kwani wakiripoti mapema watapata fursa ya kuzoea mazingira na kuanza masomo kwa wakati" amesema .
Katika hatua nyingine DC Kassanda amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika mitiani yao ya mwisho pasipo kusikiliza vishawishi ili kuunga mkono uwekezaji wa serikali katika sekta ya elimu na kuleta maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Magu Mathew Kabuta ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa miundombinu kwaajili ya wanafunzi wa kidato cha tano .
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wa kidato cha tano shule ya Sekondari Mgu , Gideon R. Ayo amesema wameridhishwa na mazingira ya shule kwani ina miundombinu yote na huduma muhimu kama maji , umeme na chakula inapatikana hivyo amewahamisisha wanafunzi wenzake kuripoti shule ili waanze masomo pamoja.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa