CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) wilaya ya Magu kimefanya mkutano wa mwaka wa wanachama wake katika matawi ya Sanjo na Ndagalu ambapo viongozi wa chama hicho wamewasisitiza wanachama umuhimu wa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi na kwa kuzingatia sheria za Utumishi wa Umma.
Akizungumza katika mkutano huo, Wakili wa TALGWU Kanda ya Ziwa Ibrahimu Zambi aliwakumbusha wanachama kuwa haki huenda sambamba na wajibu, hivyo ni lazima kudai maslahi kwa njia halali huku wakitekeleza wajibu wao ipasavyo.

“Ni muhimu kutunza siri za serikali na kuepuka uvujishaji wa nyaraka nyeti kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo ni kosa kisheria,” aliongeza.
Aidha, aliwataka wanachama kuwa mfano wa kuigwa kazini kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kufanya kazi kwa bidii na kuheshimu mamlaka zilizopo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TALGWU Mkoa wa Mwanza Mkama Sululu aliwataka wanachama wa chama hicho kuepuka kufanya mambo ambayo yanaweza kuleta shida katika ajira zao huku akisisitiza kuzingati sheria na taratibu za utumishi wa umma.

Naye, Afisa Utumishi wa Halmashauri alieleza kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana na TALGWU kulinda na kutetea maslahi ya watumishi, ikiwa ni sehemu ya kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Wanachama walipongeza juhudi za chama na uongozi wa Halmashauri kwa kuendelea kusikiliza changamoto zao na kuweka mazingira bora ya kazi.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa