ZAIDI ya watendaji 250 wa vijiji na kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu wamepatiwa mafunzo maalumu kuhusu matumizi ya mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya umma (NeST) ili waweze kusimamia ununuzi katika ngazi za chini (lower level) kwa ufanisi.
Pia mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha watendaji hao kusimamia na kuhakikisha miradi yote iliyopokea fedha kwa mwaka huu, inakamilika kabla ya tarehe 30 Juni.
Mafunzo hayo yamefanyika leo Jumanne mjini Magu mkoani Mwanza na kuratibiwa na Idara ya ununuzi ya Halmashauri hiyo.
Akifungua mafunzo hayo ambayo pia yamehusisha maafisa ununuzi ngazi ya chini, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Kyande amewataka watendaji hao kuhakikisha wanaelewa vyema sheria na taratibu zote za manunuzi ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati.
Naye Mkuu wa Idara ya Manunuzi, Hilda Mwangamila amesema mafunzo hayo pia yanalenga kuwawezesha watendaji hao kuelewa vyema sheria, kanuni na miongozo ya ununuzi kama inavyotolewa na PPRA.
“Watendaji hawa ndio jicho letu katika ngazi ya chini kabisa, hivyo tunaamini mafunzo haya yataongeza tija katika utekelezaji wa jukumu la ununuzi,” amesema.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa