Watendaji wa Kata na Vijiji Halmashauri ya Wilaya ya Magu wametakiwa kusimamia ulinzi na usalama kwenye maeneo yao kwa kuwashirikisha wananchi kikamilifu ili kusaidia kupata taarifa na kuripoti kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mohamed Ramadhani wakati wa kikao kazi kilichohusisha watendaji wa kata na vijiji wa Halmashauri hiyo kilicholenga kuwakumbusha majukumu yao ikiwemo ulinzi na usalama, usimamizi wa miradi ya maendeleo, usafi pamoja na masuala mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao.
Akizungumza wakati wa kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu amesema Watendaji wanatakiwa kua viunganishi kati ya Wananchi na Serikali katika suala la ulinzi na usalama kwani hali ya ulinzi ya Wilaya inategemea na hali ya usalama kuanzia ngazi za chini hivyo ni vyema wakasimamia vizuri suala hilo ili kuzuia vitendo vya kihalifu.
Aidha Mkurugenzi Mohamed amewahimiza watendaji hao kua na mikakati wa kutoa elimu ya lishe katika Mitaa wanayoyaisimamia ili kupunguza tatizo la udumavu.
Vilevile amewasisitiza Watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji wa mapato kwa uaminifu kwani Halmashauri inategemea makusanyo ya ndani katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo watendaji hao wanapaswa kua waadilifu katika suala la ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wake Afisa Elimu sekondari Wilaya ya Magu Beatrice Balige amewataka watendaji wa Kata na Vijiji kutokomeza suala la utoro wa wanafunzi katika maeneo yao kwa kushirikiana na wazazi na walimu ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa