Watendaji wa kata, wahudumu wa afya ngazi ya jamii na viongozi wa dini kutoka halmashauri ya wilaya ya Magu, wametakiwa kutumia nafasi zao kuelimisha jamii namna ya kufanya uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti lakini pia kuwa na utamaduni wa kwenda hospitali kufanya uchunguzi ugonjwa huo walau mara moja kwa mwaka.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Kyande wakati akifungua mafunzo ya siku moja kuhusu uchunguzi wa saratani ya matiti kwa watendaji kata, wahudumu wa afya ngazi ya jamii, viongozi wa dini kutoka Magu.
Mafunzo hayo yaliyotolewa leo Jumanne na Shirika la kimataifa la Jhpiego kwa kushirikiana na Pfizer Foundation katika ofisi za Halmashauri Magu zilizopo Ilungu, yamelenga kuwawezesha washiriki kuhamasisha jamii kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti mara kwa mara.
“Uchunguzi wa mapema ni kinga kubwa ya maisha, kwani saratani ya matiti ikigundulika mapema inatibika,” alisisitiza Kyande.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Magu, Dk. Mhana Raphael amesema saratani ya matiti bado ni changamoto kubwa katika jamii na imekuwa ikisababisha asilimia 23 ya vifo vitokanavyo na magonjwa hayo ya saratani huku saratani ya shingo ya kizazi ikiongoza kwa asilimia 25.
“Niwashukuru Jhpiego kwa sababu wanawajengea uelewa wataalam wetu kwa sababu ili tuifikie jamii kwa urahisi, tunatumia viongozi wa dini, watendaji wa kata ili kila mmoja akatimize wajibu. Tunataka kuona kila mwanajamii anajichunguza na anapima mapema, ili kupunguza athari na kuokoa maisha. Nitoe wito kwa washiriki wa mafunzo haya kwa sababu ndiyo daraja letu la kufikisha elimu hiyo kwa wananchi,” alisema.
Mradi huu unafadhiliwa na Pfizer Foundation kupitia Jhpiego na unatarajiwa kudumu kwa kipindi cha miaka mitatu mkoani Mwanza.
Aidha, washiriki wa mafunzo wameahidi kushirikiana na wataalamu wa afya ili kuifikisha elimu ngazi ya jamii, kuhimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti na hivyo kupunguza vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa