ZIKIWA zimesalia siku mbili kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu, zaidi ya wasimamizi wa vituo na wasimamizi wasaidizi wa vituo zaidi ya 2000 wameapishwa pamoja na kupatiwa mafunzo maalumu yanayolenga kuwawawezesha kusimamia uchaguzi huo mkuu.

Wasimamizi hao wameapishwa leo Jumapili tarehe 26 Oktoba, 2025 katika vituo vya Mugini - Magu mjini na Chuo cha Mipango - Kisesa ikiwa ni maandalizi kusimamia uchaguzi huo.
Aidha, akifungua mafunzo hayo mara baada ya kiapo cha utii, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Magu, Mohamed Kyande amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na miongozo inayotolewa na tume huru ya taifa ya uchaguzi.
"Jambo kubwa ambalo ninawasisitiza washiriki wa mafunzo haya ni kuzingatia sheria taratibu kanuni na miongozo ili uchaguzi uweze kufanyika kwa amani na utulivu", amesema.
Aidha, amewataka wasimamizi hao kujiepusha na kuwa vyanzo vya malalamiko au vurugu wakati wa mchakato wa uchaguzi, kufanya kazi kwa ushirikiano, kufika mapema kabla ya muda wa kufungua kituo kwa ajili ya maandalizi.

Pia amewataka kujiepusha na matumizi ya mitandao ya kijamii, kuwa nadhifu na kutumia lugha nzuri pamoja na kutoa kipaumbele kwa wapiga kura wenye mahitaji maalum pindi watakapofika kituoni.
Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mafunzo haya wamesema kuwa wanatarajia mafunzo hayo ya siku mbili watakayopatiwa yatawasaidia kutekeleza jukumu lililopo mbele kwa ufanisi mkubwa.

Wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kusimamia uchaguzi mkuu kwa huru na haki, kwa mujibu wa sheria sambamba na kuwa wazalendo huku wakiahidi kuviishi viapo vyao.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa