WASIMAMIZI Wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata katika Halmashauri ya wilaya ya Magu wametakiwa kusimamia viapo walivyokula kwa kutunza siri pamoja na kuzingatia uweledi kwa kipindi chote cha uchaguzi mkuu.
Pia wametakiwa kusimamia rasilimali vifaa watakavyopewa katika kutekeleza kazi za uchaguzi pamoja na kutoa taarifa kwa msimamizi wa uchaguzi haraka iwapo vifaa hivyo vina kasoro.
Wito huo umetolewa leo tarehe 6 Agosti, 2025 na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Magu, Mohamed Kyande wakati akifunga mafunzo ya siku tatu yaliyotolewa kwa wasimamizi hao 50 wa kata 25 za Halmashauri ya wilaya ya Magu.
“Kabla ya kuanza mafunzo haya mlikula kiapo cha kutunza siri. Kiapo kipo kwa mujibu wa kanuni namba nane ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani za mwaka 2025. Kwa hiyo ukianza kutoa taarifa za siri ambazo tume haikukupa kutoa utakuwa unatenda kosa chini ya sheria na utawajibika kwa kosa hilo.
“Sasa tunapoelekea kwenye uchaguzi kama nilivyoeleza sisi ni sehemu ya tume huru ya uchaguzi, usitumie ushabiki kutoa siri, tuwe makini na matumizi ya simu na mitandao, tuishi na viapo hivi hasa katika utunzaji wa siri na uwajibikaji,” amesema Kyande.
Awali akitoa shukrani kwa mafunzo hayo kwa niaba ya washiriki wenzake, Jackson Kadutu amesema mafunzo hayo yaliyokuwa na mada 11 yamewasaidia pia kujua maadili kuhusu uchaguzi na muda wa kampeni kuwa utaanza tarehe 28 Agosti hadi 28 Oktoba - kuanza saa mbili asubuhi hadi saa 12 jioni.
“Pia tumefahamu kuna saa za matangazo ya kampeni ambayo mwisho ni saa mbili usiku, tumefahamu taratibu hizi vizuri tunawashukuru sana wawezeshaji wetu,” amesema.
Naye Afisa Uchaguzi Jimbo la Magu, Masunga Mwagala aliwaasa washiriki hao kutekeleza majukumu yao kwa uweledi na kuweka kando itikadi za kisiasa katika maeneo yao.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa