WAKATI maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka 2025 yakiendelea kupamba moto, jumla ya wasimamizi 50 wa uchaguzi ngazi ya kata katika Halmashauri ya wilaya ya Magu wametakiwa kuzingatia katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria na miongozo ya Tume ya Huru ya Uchaguzi ili kutekeleza majukumu yao kwa uweledi.
Maagizo hayo yametolewa leo tarehe 4 Agosti, 2025 na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Magu, Mohamed Kyande wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi hao wa kata 25 yanayofanyika Magu Mjini mkoani Mwanza.
“Masharti ya Ibara ya 74(vi) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, INEC ndio inajukumu la kusimamia na kuratibu uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani Tanzania bara. Kwa hiyo ninyi mmeteuliwa kwa mujibu wa sheria na uteuzi wenu unawakilisha uwepo wa INEC katika maeneo yenu ya uteuzi.
“Hivyo mnatakiwa kuzingatia taratibu na miongozi inayotolewa mara kwa mara na tume. Lakini pia katika mafunzo haya kutakuwa na mada 11, tunawasisitiza msome kwa makini ili muweze kutekeleza majukumu haya kwa ufanisi,” amesema.
Aidha, Msimamizi msaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo Magu, Hilda Mwangamila akizungumza kwa niaba ya wasimamizi hao, ameahidi kuzingatia miongozo hiyo huku akiwakumbusha wenzie kufuatilia mafunzo hayo kwa umakini.
Naye Afisa Uchaguzi Jimbo la Magu, Masunga Mwagala akiwasilisha mada kuhusu Wajibu, majukumu na mambo muhimu ya kuzingatiwa na waratibu na wasimamizi wa uchaguzi, amewaasa kuepuka makosa ambayo baadhi ya watendaji wa uchaguzi wamekuwa wakiyarudia wakati wa uchaguzi.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa