Wananchi wa Wilaya ya Magu wametakiwa kulinda na kutunza miradi inayotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Wananchi Wilayani humo ili iweze kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo kwa maendeleo endelevu.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Magu Rachel Kassanda wakati wa Kikao cha Halmashauri kuu ya Chama cha Mapinduzi ( CCM) Wilaya ya Magu ambapo aliwasilisha utekelezaji wa Ilani ya CCM iliyomalizika Mwezi wa sita.
Akizungumza wakati wa kikao hicho DC Kassanda amesema kuwa ni vyema wananchi wakaitunza miradi hiyo ili iweze kuhudumia wananchi kwa muda mrefu kwani wasipoitunza inaweza kudumu kwa muda mfupi na kupelekea wananchi kukosa huduma muhimu.
Aidha DC Kassanda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo Wilayani Magu hususani katika sekta ya Elimu , Afya, Maji ambayo imesaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Magu Boniventura Destery Kiswaga amesema kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa mwakani viongozi wa CCM ambao wanawajua vizuri wananchi wanatakiwa kuchagua viongozi wazuri wanaokubalika na wananchi ili kuwatumikia na kuwaletea maendeleo.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa