Mkuu wa Wilaya ya Magu, Rachel Kassanda amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa ( El-Nino) zilizotabiriwa kunyesha kuanzia mwezi Oktoba 2023 baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa kutoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za vuli ambao umetabiri uwepo wa El- Nino .
DC Kassanda ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Lumeji Kata ya Sukuma Wilayani Magu ikiwa ni muendelezo wa Ziara zake za Kata kwa kata kwaajili ya kusikiliza na kupokea kero za Wananchi na kuzipatia ufumbuzi.
Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho DC Kassanda amewaasa Wananchi wanaokaa maeneo ya bondeni kutengeneza mazingira ya kuchukua tahadhari mapema ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo vifo na uharibifu wa mali.
" Nawaomba Wananchi tuchukue tahadhari mapema na kutengeneza mazingira yakae sawa haswa wakazi wa maeneo ya bondeni kwani utabiri wa mamlaka ya hali ya hewa umeonesha mvua za mwaka huu zitakua kubwa hivyo tahadhari ni muhimu.
Aidha DC Kassanda amewataka viongozi wa ngazi ya kata na vijiji kutoa elimu kwa wananchi wao ili wachukue tahadhari mapema.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa