WAGOMBEA watatu kutoka vyama vya AAFP, SAU na Demokrasia Makini wamejitokeza leo Ijumaa kuchukua fomu za uteuzi wa kugombea ubunge katika jimbo la Magu mkoani Mwanza.
Wagombea hao Daniel Nko (AAFP), Neema Lameck Onduta (SAU) na Eva Henry (Demokrasia Makini), wamekabidhiwa fomu hizo na Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Magu, Mohamed Kyande.
Hatua hiyo inajiri baada ya Tume Huru ya Taifa Uchaguzi (INEC) jana Alhamisi kutangaza kuwa kuanzia tarehe 14 Agosti, 2025 hadi tarehe 27 Agosti, 2025 Wasimamizi wa Uchaguzi wa majimbo wataanza kutoa fomu za uteuzi wa wagombea Ubunge katika Jamhuri ya Muungano na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya kata wataanza kutoa fomu za uteuzi wa wagombea Udiwani kwa Tanzania Bara.
“Hivyo, wanachama wa vyama vya siasa waliopendekezwa na vyama vyao kugombea nafasi ya Ubunge kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wafike katika ofisi za Wasimamizi wa uchaguzi wakiwa na barua za utambulisho kutoka 1 B katika vyama vyao kuanzia saa moja na nusu (1:30) asubuhi hadi saa kumi kamili (10:00) alasiri,” alisema Mkurugenzi wa INEC, Ndugu, Kailima Ramadhani.
Aidha, kwa wanachama waliopendekezwa kugombea nafasi ya Udiwani kwa Tanzania Bara wafike katika ofisi za Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya kata wakiwa na barua za utambulisho kutoka katika vyama vyao kuanzia saa moja na nusu (1:30) asubuhi hadi saa kumi kamili (10:00) Alasiri.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa