MAOFISA uandikishaji katika daftari la uchaguzi wa serikali mitaa wametakiwa kuzingatia kanuni na sheria za uchaguzi huo pamoja na kuwa waadilifu ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Wito huo umetolewa jana tarehe 8 Oktoba, 2024 mjini Magu mkoani Mwanza na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhan Kyande wakati akiwaapisha waandikishaji hao.
Alisema kiapo walichoapa waandishikishaji hao ndio kitanzi chao hivyo wanapaswa kuzingatia maadili na sheria za uchaguzi huo ili kuondoa malalamiko yoyote yanayoweza kujitokeza.
“Niwapongeze kushiriki kwenye semina, uteuzi wenu umepitia hatua mbalimbali za upembuzi hivyo mmepitia kwenye tanuru la moto kwelikweli, lakini pia walioachwa sio kwamba hawakuwa na uwezo bali nafasi ni chache hivyo tukafanya kazi kwa uweledi na uadilifu mkubwa,” alisema.
Naye Afisa Uchaguzi wilaya ya Magu, Mwagala Masunga alisema zoezi la kuandikisha wapiga kura uchaguzi huo litaanza tarehe 11 hadi 20 Oktoba mwaka huu huku kampeni zikitarajiwa kuanza tarehe 20 hadi 26 Novemba mwaka huu.
Aidha, aliwaonya waandikishaji hao kuandikisha wananchi wote kwenye vitongoji vya bila kujali itikadi zao za vyama.
“Tushirikiane kukamilisha zoezi hili. Mkihitaji maelekezo msisite kuwasiliana na ofisi yangu,” alisema.
Alisema uchaguzi huo utafanyika katika mamlaka mji mdogo wa Magu Pamoja na wilaya ya Magu ambapo kwa ujumla kuna vijiji 82 na vitongoji 508.
Alisema viongozi wanaochaguliwa katika ngazi hizo ni wenyeviti wa vijiji, wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji, wenyeviti wa mitaa, wajumbe wa kamati za mitaa na wenyeviti wa vitongoji.
Zoezi la kujiandikisha litazinduliwa rasmi tarehe 11 Oktoba, 2024 na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ilihali uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa, unatarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba mwaka huu, kote nchini.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa