KATIKA kutimiza malengo ya upandaji miti milioni 1.5, Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza imepokea miche ya miti 100,000 kutoka kwa Kampuni ya huduma kwa wateja - Via Aviation pamoja na Chama cha Madereva Pikipiki nchini (CHAMWAPITA).
Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa awamu ya kwanza ya miti hiyo iliyofanyika leo Jumanne kwenye Shule ya Sekondari ya wasichana Mwanza, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Via Aviation, Susan Mashibe amesema katika shule hiyo wametoa miche ya miti 5000.
“Kwa wilaya ya Magu tumeanza na miche 100,000 kati yake miche 5000 tumeleta hapa Mwanza Girls. Tumewaletea miche ya miti ya aina mbalimbali ikiwemo ya matunda, mbao, vivuli na urembo.
“Lengo letu ni kugawa miche milioni moja ya miti kwa mwaka kwenye wilaya mbalimbali za kanda ya ziwa hasa ikizingatiwa jamii za watu wa ukanda huu zinategemea zaidi nishati ya mkaa na kuni katika kupikia,” amesema.
Naye Naibu Katibu wa CHAMWAPITA, Joseph Nsabila amesema wamechangia miti 3000 kwa shule hiyo ili kuunga mkono hamasa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya uhifadhi wa mazingira.
Aidha, Katibu Tawala wa halmashauri hiyo, Jubilate Lawuo ameishukuru kampuni hiyo ya VIA aviation kwa kuendana na kampeni ya Rais Samia ya uhifadhi mazingira ikiwamo upandaji wa miti.
“Kama wilaya tumeandaa miche milioni 1.5 kwa sababu nakumbuka wakati nafika Magu, ilikuwa wilaya ya jangwa… hapakuwa na miti lakini sasa hali ni nzuri, cha msingi tuendelee kustawisha miti,” amesema.
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Rehema Samson alishukuru shule yao kupatiwa miti hiyo kwa sababu wa sababu tutapata faida nyingi ikiwemo matunda na mazingira mazuri.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa