MKUU wa Wilaya ya Magu, Jubilate Lawuo ameitembelea familia ya Mzee Shadrack Ntagala (66) iliyopata ajali ya moto na kuipa pole huku akiwasisitiza wananchi kuchukua tahadhari ya matumizi ya vifaa vya umeme na kutoa taarifa haraka tatizo linapotokea.
Katika ajali hiyo ya moto iliyotokea saa sita usiku wa kuamkia leo maeneo ya mtaa wa National kata ya Magu Mjini wilayani Magu, jumla ya watu watatu wa familia hiyo wamefariki dunia huku baba wa familia akinusurika.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Zimamoto na Uokoja Wilayani Magu, Inspekta Gaston Tibulebwa katika nyumba hiyo iliyokuwa na watu wanne, waliofariki ni Mwakebeta Mathew (62) ambaye ni mke wa Ntagala, Liberate Ngwata (40) ambaye ni dada wa Ntagala pamoja na Neema Festo Kizinga (18) ambaye ni mjukuu na mwanafunzi wa kidato cha tatu Magu Sekondari.
Amesema mzee Ntagala amenusurika baada ya kuokolewa na kijana aliyekuwa amelala nyumba ya jirani. Kijana huyo alifanikiwa kuvunja mlango wa nyumba hiyo na kumtoa mzee huyo ambaye sasa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza.

Awali DC Lawuo akizungumza na wanafamilia pamoja na wananchi waliofika kuomboleza, mbali na kuwapa pole wafiwa, amelipongeza jeshi la zimamoto na uokoaji wilaya ya Magu kwa kufika kwa wakati na kusaidia kuzima moto huo usilete madhara zaidi.
“Ndugu zangu Wana-Magu tunatakiwa kuwa makini na mali zetu, ukiona tukio lolote tupeane taarifa mapema ili uharibifu mkubwa kama huu usitokee.

“Inspekta Gaston amekuwa akitoa namba za simu kwa wananchi wote ili kunapotokea tukio wakati wowote mtoe taarifa, lakini pia niwaombe kuchunguza vifaa vya umeme tunavyovitumia, tusitumie cable moja kwenye matumizi ya vifaa vyote vya ndani, ikizidiwa inapata joto na kuungua,”
Aidha, akielezea tukio hilo dada wa Ntagala, Mwinjilisti Marry Yona amesema taarifa za tukio hilo amezipata saa 10 usiku wa kuamkia leo wakati akiwa kwenye shughuli zake katika kata jirani ya Nyanguge.
Akielezea hali ya kaka yake amesema, majeruhi huyo anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa kanda Bugando hivyo wanaendelea kuangalia hali yake ndipo watajua taratibu za mazishi ya wapendwa wao ambao miili yao imehifadhiwa katika mochwari hospitali ya wilaya ya Magu.
Naye kijana Mashaka Mabula ambaye ndiye aliyekuwa wa kufika kwenye tukio na kumuokoa Mzee Ntagala, amesema alijulishwa kuhusu tukio hilo na mama mmoja wa jirani.
“Alikuja kunigongea na kuniambia kuna moto unawaka kwenye nyumba wa baba wa familia. Nikaenda kuvunja mlango nikakuta mzee yupo mlangoni nikamtoa ndipo nikaanza kuzima moto kwa kuunganisha mpira wa maji kwenye bomba lililo hapa nje,” amesema na kuongeza kuwa baada ya muda kidogo ndipo askari wa zimamoto na uokoaji walikuja na kusaidia kuzima moto huo.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa