Halmashauri ya wilaya ya Magu itaendelea kulinda na kutetea haki za wanawake pamoja kuelimisha jamii kuwajibika ipaswavyo katika kuwasaidia na kuwahudumia waathirika wa ukatili.
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Magu Jubilate win Lawuo wakati akizundua jukwaa la uwezeshaji wa wanawake kiuchumi tarafa ya itumbili katika ukumbi wa CCM Wilaya ya Magu uliopo kata ya Magu Mjini.
Akizungumza wakati akizindua jukwaa hilo Katibu Tawala Lawuo amesema kuwa Msingi wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ni kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 – 2025 ya Chama Cha Mapinduzi inayoelekeza kuwainua Wanawake Kiuchumi kwa kuwapatia fursa mbalimbali kwa kuwaunganisha wanawake kwenye mafunzo, kuwaunganisha wanawake na fursa za kilimo, kuwaunganisha wanawake na mikopo yenye masharti nafuu.
"Jamii yetu lazima itambue kuwa Wilaya yetu ya Magu inatekeleza na inamuunga mkono Mh. Rais wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fursa mbalimbali zinazopatikana nje na ndani ya Wilaya ya Magu" amesema .
Aidha Katibu Tawala huyo amewaomba wananchi wote wa Wilaya ya Magu kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata, viongozi wa madhehebu ya dini, viongozi wa vyama vya siasa na kila mtu kwa nafasi yake kuendelea kulaani na kukumea kwa nguvu zetu zote vitendo vyote vya ukatili vinavyotokea katika maeneo yote ya Wilaya.
"Hakika tunahakikisha Magu yetu itamkomboa mwanamke kwa kuongeza wigo mpana kwa kuwaunganisha wanawake na wadau, pia Halmashauri kuweza kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu baada ya dirisha la utoaji mikopo kufunguliwa" ameongeza
Katika hatua nyingine Katibu Tawala Lawuo amesema Serikali itahakikisha kunakuwa na Miundombinu wezeshi kwa wanawake na wanajamii wote ikiwa ni pamoja na kuwa na miradi mikubwa ya kilimo cha umwagiliaji ambayo itaongeza uzalishaji wa zao la Mpunga na pia kuongeza ajira kwa vijana.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa