Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mh. Simon Mpandalume amewataka watumishi wa Halmashauri hiyo kuendelea kua na ushirikiano, umoja, uadilifu na weledi ili kufikia lengo la kukusanya Bilioni 4.5 za mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2023-2023 .
Mh Mpandalume ameyasema hayo wakati wa mkutano wa baraza la madiwani kwaajili ya kupitia taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kipindi cha robo ya kwanza Julai- Septemba, 2023-2024 uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa CCM Wilaya ya Magu Leo Jumatano Novemba 08, 2023.
Akizungumza wakati wa mkutano huo Mh. Mpandalume amesema kuwa bajeti hiyo ni kubwa na ili kufikia lengo ni muhimu watumishi kwa kushirikiana na viongozi kuanzia kazi ya chini kufanya kazi kwa ushirikiano na kusimamia ukusanyaji wa mapato.
" Tunahitaji weledi na uwajibikaji wetu sote baraza la madiwani, watendaji wetu kuanzia ngazi za chini kwenye vijiji hadi Wilaya ili tufikie malengo ya kukusanya mapato haya" amesema
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Bi Fidelica G. Myovella amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa ( El-Nino) zilizotabiriwa kunyesha kuanzia mwezi Oktoba 2023 baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa kutoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za vuli ambao umetabiri uwepo wa El- Nino .
Myovella amesema Wananchi wanaokaa maeneo ya bondeni ni vyema wakaendelea kutengeneza mazingira ya kuchukua tahadhari mapema ikiwemo kuhama katika maeneo hayo ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo vifo na uharibifu wa mali.
" Wazazi hakikisheni watoto hawachezi kwenye madimbwi na maeneo ya kingo za mito ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza " amesema
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa