Mkuu wa Wilaya ya Magu, Mheshimiwa Dkt. Philemon Sengati (PhD), leo tarehe 20.03.2019 amekabidhi matrekta 13 kwa vyama vya msingi vya ushirika, yaliyotolewa na Serikali kwa njia ya mkopo kupitia Benki ya Maendelo ya kilimo (TADB). Matrekta hayo yalikabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa.
DC Sengati amesema kuwa Wilaya ya Magu inatarajia kupatiwa jumla ya matrekta 33 ambayo yanatolewa kwa awamu tatu, 13 tayari yamekabidhiwa, 12 yatakuja awamu ya pili na 8 yatatolewa awamu ya tatu. Pia amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uzalendo wake dhamira na ndoto yake ya kulipeleka Taifa katika uchumi wa kati wa Viwanda. “Hivyo ili viwanda vifikiwe lazima tuwekeze katika kilimo ambacho ndicho huzalisha mali ghafi kwa ajili ya viwanda. Matrekta yataenda kufanya mapinduzi makubwa katika Kilimo na tutalima kwa tija na kuongeza kasi ya uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara”.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Lutengano George Mwalwiba ameipongeza Serikali kwa kutoa matrekta kwa Wakulima kitendo ambacho kitachochea ukuaji wa uchumi kwa Wanamagu, na kuwaondoa wananchi katika kilimo duni cha jembe la mkono vilevile ameshukuru watendaji wa Idara ya kilimo, umwagiliaji na ushirika kwa kuhamasisha uanzishwaji wa vyama vya ushirika ambapo kwa mwaka jana vilifanya vizuri kwa mkoa wa Mwanza pia kwa kuratibu vizuri mchakato wa upatikanaji wa matrekta hayo.
Vyama vya ushirika vilivyopewa kwa awamu ya kwanza ni Igunabalimi (Jinjimili), Masengese (Kabale), Nhobola, Ndagalu, Chandulu, Mahaha, Shishani, Nsobu (Nsola Bubinza) Mwalinha, Lugeye, Nyanguge, na Bugatu. DC Sengati amewataka viongozi wa vyama vya ushirika kusimamia vizuri vyombo hivyo kwa mujibu wa taratibu na kwamba viziwe chanzo cha migogoro na vikatumike kwa maslahi mapana ya jamii na wanachama wa vyama hivyo. Pia amewaasa kufuata vigezo walivyopewa ikiwemo kufanya marejesho kwani mkopo huo umetolewa kwa asilimia mia moja kwa udhamini wa Serikali.
Nao viongozi wa vyama vya ushirika wameipongeza Serikali kwa utendaji kazi wake uliotukuka, “kwa Kweli Matrekta haya yanaenda kuamsha ari ya wakulima kupanua zaidi shughuli zetu za kilimo na kusaidia kuondakana na umasikini na Tunawaahidi kuwa tutafanya kazi kwa uaminifu kama Serikali ilivyotuamini” Amesema Mwenyekiti wa AMCOS Mahaha.
Magu Kazi na Maendeleo- Kusema na kutenda
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa