MWENGE wa Uhuru leo Jumamosi umezindua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi Igudija uliogharimu kiasi cha Sh milioni 540.3 fedha kutoka Serikali Kuu kupitia Programu ya BOOST.
Mradi huo unajumuisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 16, matundu ya vyoo 24, jengo la utawala moja utengenezaji wa madawati 210 ya elimu msingi, meza 30 za elimu ya Awali pamoja na viti vyake 30, viti vya walimu 14 na meza 17.
Mradi huo uliotekelezwa kwa kutumia utaratibu wa ‘‘Force Account’’ na kukamilika kwa asilimia 100 na unaendelea kutoa huduma, umezinduliwa na Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa, Godfrey Mzava mbele ya mkuu wa wilaya ya Magu, Joshua Nassari na viongozi wengine wa halamshauri waliohudhuria mbio hizo za mwenge.
Awali Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Benifaxad Chiguru amesema kukamilika kwa mradi huo kumesaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule za Kisesa, Muungano, Wita, Igekemaja na Kitumba.
Aidha, mmoja wananachi wenye Watoto wanaosoma katika shule hiyo, Prisca Revocatus ameishukuru Serikali kwa ujenzi wa shule hiyo ambayo imekuja kuondoa changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kwenda shule ya msingi Kisesa na kuwaepusha na ajali zilizosababishwa na kuvuka barabara.
Naye Mwenyekit kamati ya shule, Abel Elikana amesema ujio wa shule hiyo mpya kutapunguza pia ajali za barabarani kwani watoto kwa sasa hawavuki barabara kuelekea upande wa pili kufuata huduma ya elimu huku na miti 800 ikiwa imepandwa kuzunguka eneo la shule ili kuhakikisha mazingira yanatunzwa.
Awali kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mzava amesema Rais Samia Suluhu Hassan anawapenda wananchi wake na anaendelelea kuamini kuwa urithi wa mtoto ni elimu ndio maana akaridhia kutolewa kwa fedha hizo kwa kuwajengea shule mpya ya awali na msingi kwenye kijiji cha Idugija badala ya kuchangisha wananchi.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa