MWENGE wa Uhuru umepokewa leo tarehe 27 Agosti, 2025 wilayani Magu kutokea wilayani Ilemela na unatarajiwa kupitia miradi nane yenye thamani ya Sh bilioni 2.
Akipokea Mwenge huo katika hafla iliyofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Kisesa, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Jubilate Win Lawuo amesema Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Wilaya ya Magu utakimbizwa umbali wa kilomita 110 toka eneo la mapokezi hadi makabidhiano.
“Aidha, Mbio za Mwenge wa Uhuru zitazindua miradi 8 yenye thamani ya shilingi 2,014,635,515.00, kati ya miradi hiyo mradi mmoja unatokana na mapato ya ndani.
“Katika miradi hii, Jamii imechangia kiasi cha Tsh. 768,753,600.00, Halmashauri Tsh. 100,322,350.00, Serikali Kuu Tsh. 896,469,685.00 na wahisani Tsh. 249,089,880.00,” amesema Lawuo
Akizungumza baada ya kutembelea miradi hiyo ikiwamo mradi wa uhifadhi wa mazingira na matumizi ya nishati safi ya kupikia, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2025 Bw. Ismail Ali Ussi amepongeza halmashauri ya Magu kwa kutekeleza kwa vitendo maagizo ya serikali kuhusu mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akikagua mradi wa uhifadhi wa mazingira na utumiaji wa nishati safi na salama katika shule ya sekondari ya wasichana Mwanza, Ussi amesema hilo ni moja ya jambo ambalo Rais Samia amekuwa akilisisitiza ili kulinda afya za wananchi na uhai wa mazingira kwa ujumla.
Akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge, Mkuu Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira, Ngusa Buyamba amesema mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 13.2 kati yake Shilingi milioni 6.4 zimetumika kusimika mfumo wa nishati safi na salama ya kupikia katika Shule hiyo.
Akiwa katika mradi kikundi cha vijana cha Waosha magari Kisesa, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2025 amejonesha shughuli zinazofanywa na kikundi hicho na kusisitiza vikundi vingine kuendelea kuchangamkia mikopo hiyo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.
Kwa upande wake katibu wa kikundi cha waosha magari Kisesa, John Jacob amesema Mradi huo umegharimu kiasi cha Shilingi Milioni 30 kati ya hizo Milioni 20 mkopo wa vijana kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Magu uliotolewa tarehe 19/03/2025 na Milioni 10 ni fedha za wanakikundi na kufafanua kuwa Kikundi kinatarajia kukamilisha marejesho ya mkopo huo tarehe 19/03/2028.
Mbio hizo za Mwenge wa Uhuru pia zimezindua Zahanati katika kijiji cha Nyashimba wilayani Magu iliyojengwa kwa Tshs. Milioni 92.2 kutoka chanzo cha makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo.
Akizungumza na maelfu ya wananchi waliojitokeza kuipokea zahanati hiyo, Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa 2025 Bw. Ismail Ali Ussi amewapongeza Viongozi wa Halmashauri na Wilaya hiyo kwa kutoa fedha ambapo amesema zitasaidia kuboresha huduma hususani za mama na mtoto na kupelekea kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Aidha, Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi pia amekagua mradi wa lishe uliopo wilayani humo na kuwapongeza wajasiriamali waliowekeza katika mradi huo wa lishe kutokana na ubunifu wa bidhaa zao.
“Mradi huu wa lishe ni miongoni mwa miradi inayotekelzwa na wazawa, hiki ndicho Rais Samia Suluhu Hassan anachotuhamasisha sisi Watanzania kuwa wabunifu. Nimeshuhudia bidhaa mbalimbali zenye viwango vya juu zinazolishwa na wajasiriamali hawa, tunawashukuru sana kwa sababu ni kazi zinazoendana na wakati,” amesema.
Awali akisoma taarifa kuhusu mradi huo mbele ya kiongozi huyo wa mbio za Mwenge, Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Magdalena Lema amesema Wilaya ya Magu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya lishe inaendelea kusimamia kikamilifu suala la lishe bora kwa wananchi wote.
Mbali na mradi wa lishe pia mbio hizo za Mwenge wa uhuru zimezindua barabara yenye kiwango cha lami iliyopo katika mji wa Magu.
Mradi huo wa matengenezo ya barabara kiwango cha lami (RC Hostel) yenye urefu wa Kilomita 0.38 iliyopo katika Mji wa Magu, ulitekelezwa kwa kupitia fedha za mfuko wa Jimbo, ulitekelezwa na Mkandarasi Mzawa ASA GENERAL SUPPLIES & CONSTRACTION CO. LTD wa kutokea Bunda.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge ameupongeza uongozi wa halmashauri kwa kusimamia vema miradi ya maendeleo kutekelezwa kwa ufanisi.
Aidha, amewataka wananchi kuilinda miradi hiyo hasa ikizingatiwa inawanufaisha wao katika kujieletea maendeleo.
Awali akisoma taarifa mbele ya kiongozi huyo wa mbio za Mwenge, Meneja TARURA wilaya ya Magu, Eng Musa Mzimbiri amesema lengo la matengenezo ya barabara hiyo kwa kiwango cha lami nyepesi ni kuweza kupitika katika misimu yote ya mwaka ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji na pia kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi kwa kipindi chote cha mwaka.
Mwenge wa uhuru pia umezidua Mradi wa maji Njicha kijiji cha Ihayabuyaga upo kwenye kata ya Bukandwe kilomita 40 kutoka yalipo Makao Makuu ya Wilaya ya Magu.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa