MTHIBITI Ubora Mkuu wa Wilaya ya Magu, Hilda Mushi amewataka wazazi wajitokeze kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni pamoja na kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ya shule ikiwamo michango ya chakula kwa ajili ya watoto wao pindi wawapo shuleni.
Pia amewataka wamiliki wa shule zote katika wilaya hiyo kuhakikisha wamesajili shule zao ili wasikumbane na mkono wa sheria pindi wanapoendelea kutoa huduma hiyo.
Wito huo umetolewa leo tarehe 7 Machi, 2025 na Mthibiti huyo mkuu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu majukumu ya ofisi hiyo.
“Ninawaomba wazazi wajitoe kushirikiana na walimu kusimamia masuala mbalimbali ya watoto wao ikiwamo kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni, pia wajitokeze kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ya shule kwa mfano suala la chakula.
“Wazazi ni wagumu kuchangia ila ukweli ni kwamba huwezi kumfundisha mtoto mwenye njaa,” amesema.
Akizungumzia adhabu zinazotolewa na walimu kwa wanafunzi, Mushi amesema ofisi yake imekuwa ikitoa elimu kwa walimu mara kwa mara kwamba elimu haitolewi kwa adhabu.
“Cha msingi ni kuzungumza na mtoto, lakini mtoto analelewa na pande zote kati ya mwalimu, mzazi na jamii husika hivyo ili kufuatilia nidhamu pia ya wanafunzi tunaomba wazazi watoe ushirikiano.
Aidha, akifafanua kuhusu mitaala iliyoboreshwa mwaka 2022/2023, Mthibiti ubora wa wilaya hiyo, Said Habibu amesema tayari serikali imejipanga kuendana na maboresho hayo ikiwamo kuandaa walimu pamoja na shule zenye nyenzo za kutosha kuwaandaa wanafunzi hao.
“Maboresho yanalenga kuwa na wahitimu wenye maarifa na ujuzi na kushinda katika soko la ajira duniani,” amesema.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa