Mkuu wa Wilaya ya Magu Rachel Kassanda anaendelea na ziara ya kukagua shughuli mbalimbali za miradi ya maendeleo Wilayani humo Leo ametembelea mradi wa maji majibomba Chabula- Bugando unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA kwaajili ya kujionea maendeleo ya mradi huo unaotarajia kuondoa changamoto ya maji katika vijiji vinne .
Mradi huo ambao chanzo chake cha maji ni Ziwa Victoria ulianza kujengwa mwaka 2019 na unatekelezwa na MWAUWASA na unahudumia vijijini Vinne ambavyo ni Chabula, Bugando, Nyashigwe na Kongolo ambapo jumla ya Wananchi wapatao 21,400 watahudumiwa na mradi huu.
Akisoma taarifa ya mradi mbele ya Mkuu wa Wilaya Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Magu Mhandisi Daud F. Amlima amesema kuwa mradi huu umetekelezwa kwa ushirikiano kati ya wataalamu wa MWAUWASA na wataalamu wa RUWASA Wilayani Magu.
Kuhusu Gharama za mradi mhandisi Amlima amesema mradi umetekelezwa kwa Tsh. 1,786, 740,139.00 na fedha zilizotumika hadi sasa ni Sh. 1,776,740,139.00 ambapo utekelezaji wa mradi huu ulianza Mwezi April , 2020 na umekamilika Mwezi July 2023.
Akifafanua kuhusu maendeleo ya mradi huo amesema kwa sasa uko katika hatua za majaribio ili kuona kama vituo vyote 31 vinapata maji pamoja na kuangalia mapungufu ya miundombinu yote iliyojengwa ili kuangalia mapungufu ya miundombinu yote iliyojengwa na kuifanyia marekebisho.
Amesema kuwa baada ya wiki moja wananchi wataanza kutumia maji ingawa wakati huu wa majaribio wananchi wanaendelea kutumia maji.
Katika Ziara hiyo DC Kassanda aliambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Magu Bi. Fidelica G. Myovella , Kamati ya ulinzi na usalama na wakuu wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa