Halmashauri ya Wilaya ya Magu imepokea Mwenge wa Uhuru Tarehe 27.08.2018 katika kijiji cha Mwamabanza. Mwenge huo umefungua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi Milioni 979.5 na umekimbizwa umbali wa km 97. Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa ndugu Charles F. Kabeho ameikubali miradi yote na kusema imetekelezwa kwa kiwango kwani thamani ya fedha (Value for Money) imeonekana katika miradi hiyo.
Aidha katika ujumbe wa Mwenge 2018, amesema “Elimu ni ufunguo wa maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya taifa letu”, Serikali inatoa elimu msingi bila malipo kwa maana ya kuondoa michango yote kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne. “Wazazi wawajibike katika kuwanunulia watoto wao sare za shule na kuchangia maendeleo ya shule kama vile ujenzi wa miundombinu na kuhakikisha kua kunakuwepo na upatikanaji wa chakula shuleni kwa kuzingatia waraka wa elimu Namba 3 wa Mwaka 2016 unaotaka michango yote inayohusu maendeleo ya shule iratibiwe na wananchi/wazazi wenyewe” amesema Kabeho.
“Serikali imedhibiti suala la utoro wa wanafunzi kwani Mkoa wa Mwanza hauna utoro uliokithiri japo kuna utoro wa kiholela hivyo wazazi wasimamie watoto wao kwenda shule. Pia Serikali imegawa vifaa vya maabara katika shule za sekondari 1625 kwa ajili ya kusaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo ambapo kila shule ya sekondari inatakiwa iwe na maabara zote za Masomo ya Sayansi”, amesema Kabeho.
Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa amewakabidhi hundi za mikopo ya wanawake na zenye Jumla ya shilingi 24,000,000.00 kwa mchanganuo ufuatao, vikundi 12 vya wanawake shilingi 17,000,000.00 na vikundi 5 vya vijana shilingi 7,000,000.00.
Kiongozi huyo amewaomba wananchi washiriki kutokomeza malaria kwa maendeleo ya jamii, kupinga Rushwa, madawa ya kulevya na kupima afya zao kwa hiari. Aidha katika mkesha wa wa mwenge uhuru Kisesa, jumla ya watu 621 wamejitokeza kupima Virusi vya UKIMWI ambapo watu 11 wamegunduliwa kuwa na maabukizi ya VVU sawa na asilimia 1.7 ya waliopima.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa