Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mohamed Mchengerwa amewaelekeza makatibu tawala na wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha maofisa habari ambao hawajapewa ofisi au wamenyang’anywa na kupewa Idara nyingine, maofisa hao wapatiwe ofisi zao mara moja.
Pia amewaagiza kuhakikisha maofisa habari wanaokaimu ukuu wa vitengo ambao wana sifa wakabidhiwe vitengo vyao ili watekeleze kikamilifu jukumu la kuuhabarisha umma kwa usahihi.
Aidha, ameagiza vitengo hivyo kutengewa vifungu vya fedha kutoka vyanzo vya mapato ya ndani ya halmashauri au matumizi mengineyo (OC) ili watangaze mafanikio yaliyopatikana kwenye eneo la utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambalo limepewa kipaumbele na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mchengerwa ametoa maagizo hayo leo kwa Naibu Katibu Mkuu (Miundombinu) aliyemwakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Adolf Ndunguru na kumsisitiza kufuatilia utekelezaji wake haraka.
Ameonya iwapo utekelezaji huo utakwamisha na baadhi ya wajiri wakiwemo wakurugenzi wa halmashauri (DED), wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Mchengerwa ambaye amefungua kikao kazi cha Maafisa Habari wa Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi za Ofisi ya Rais-TAMISEMI Dodoma, amesema ofisa habari anatakiwa kukaimu kitengo kwa muda usiozidi miezi sita.
Pia ameelekeza Maafisa Habari wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kushiriki kwenye ziara za viongozi ili wapate uelewa utakaowawezesha kutangaza kwa ufanisi mafanikio ya Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Pamoja na mambo mengine amewataka Maafisa Habari Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika maeneo yao ya kazi.
“Mmebeba dhamana kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi hivyo msiwaache watanzania walishwe habari potofu” Mchengerwa amesisitiza.
Mchengerwa amesema Maofisa Habari nchini ni rasilimaliwatu muhimu hivyo wakitambua wajibu wao na kujiimarisha kiutendaji ni wazi kuwa wananchi watapata taarifa sahihi kwa wakati.
“Iwapo kila mmoja wenu akiwa mzalendo na kutambua wajibu wake, habari mtakazozitoa ndio zitaaminiwa na kupokelewa na watanzania kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ambayo imeshamiri hivisasa,” Mchengerwa amehimiza.
Mchengerwa amesema anaamini kwamba maofisa habari waliopo wana weledi na ujuzi unaowawezesha kutoa taarifa sahihi zenye tija kwa wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa