Mbunge wa jimbo la Magu Boniventura Kiswaga amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha shilingi Milioni 584 kwaajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari Kigangama katika Kijiji cha Kigangama kata ya Kitongosima Wilayani Magu ambayo ujenzi wake upo katika hatua za mwisho na itarajiwa kupokea wanafunzi katika mhula mpya wa masomo 2024-2025.
Mbunge Kiswaga ametoa shukrani hizo wakati wa ziara ya kamati ya mfuko wa jimbo kwaajili ya kukagua miradi iliyopelekewa fedha kwa mwaka wa fedha 2022-2023 kwa lengo la kuchochea maendeleo ya miradi mbalimbali iliyoanzishwa na wananchi katika Jimbo la Magu ambapo mfuko wa jimbo ulipeleka shilingi milioni 5, 440, 000 kwaajili ya kuchangia zoezi la ununuzi wa tofali za ujenzi wa shule hiyo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo mbunge Kiswaga amesema shule hiyo inayojengwa kupitia mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari ( SEQUIP) itasaidia kutatua changamoto ya wananfunzi kutembea umbali mrefu ambapo wanafunzi wa kata hiyo wanatembea takribani KM 7 kwenda katika shule ya sekondari Lugeye.
" Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia kwa kudhinisha pesa kwaajili ya ujenzi wa shule hii na kuona uhitaji wa wananchi kuhitaji shule katika kijiji hiki kwani wanafunzi wengi walikua wanaishia njiani kutokana na umbali hivyo tunamshukuru sana Mh. Rais kwa kuliona hili".
Aidha Kiswaga amebainisha kuwa fedha za mfuko wa jimbo zipo kwa lengo la kusaidia miradi ya wananchi iliyoanzishwa kwa manufaa ya Taifa ili iweze kukamilika hivyo akawahimiza wasimamizi wa miradi kusimamia vizuri na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika ili fedha za mfuko wa jimbo zitumike kama ilivyokusudiwa .
Kwa upande wake Afisa Mipango wa Wilaya ya Magu Pastory Mkaruka amesema katika ziara hiyo wametembelea miradi mbalimbali na kuona thamani ya fedha zilizotolewa na mfuko wa jimbo zilizvyotumika katika kuchochea maendeleo ya miradi mbalimbali iliyoanzishwa na wananchi.
Aidha alimshukuru Mbunge Kiswaga kwa jitihada za kuhakikisha fedha za mfuko wa jimbo zinapatikana na kuchochea miradi mbalimbali iliyoanzishwa na wananchi.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa