Mbunge wa Viti maalum CCM mkoani Mwanza, Marry Masanja leo Jumanne amejiandikisha katika daftari la wapiga kura wa uchaguzi wa serikali za mitaa katika kituo cha Magu kilichopo kata ya Magu Mjini wilaya Magu mkoani Mwanza.
Masanja pia amezungumza na wananchi na wafanyabiashara wa eneo hilo la stendi ya mabasi na daladala Magu na kuwaelimisha umuhimu wa kujiandikisha katika daftari hilo la uchaguzi wa serikali za mitaa.
Akizungumza na wananchi hao waliofurika katika eneo hilo kumsikiliza, Masanja ametoa rai kwa wananchi kutambua kuwa uandikishaji wa daftari la kudumu la uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Septemba, haumpi sifa mwananchi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Ili kuwa na sifa za kumchagua mwenyekiti wa kitongoji na Kijiji chako, unatakiwa kwenda kujiandikisha sasa kwenye daftari la uchaguzi wa serikali za mitaa, ten ani zoezi ambalo hutumii muda mrefu ndani ya dakika moja umemaliza kujiandikisha na kuwa na sifa ya kushiriki uchaguzi huo,” amesema.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kwenda kujiandikisha katika daftari la uchaguzi wa serikali za mitaa lililofunguliwa tarehe 11 Oktoba mwaka huu hadi tarehe 20 Oktoba ili kumchagua kiongozi atakayeungana na serikali kuwaletea maendeleo.
“Rais Samia Suluhu Hassan alijiandikisha kule Chamwino - Dodoma kwenye makazi yake na mimi nimekuja kujiandikisha kwenye makazi yangu hapa Magu Mjini maana mimi ni mtoto wa stendi.
“Napenda kutoa wito kwa wananchi kuwa wasisubiri hadi siku za mwisho ndio wajitokeze kujiandikisha badala yake wajitokeze sasa kwani zoezi halitumii muda mrefu, ndani ya dakika moja unakuwa umemaliza kujiandikisha,” amesema.
Kwa mujibu wa Afisa Uchaguzi wilaya ya Magu, Mwagala Masunga, zoezi la kujiandikisha katika wilaya ya Magu linaendelea vizuri hasa ikizingatiwa kwa muda wa siku nne, tayari wananchi 95,157 wamejiandikisha.
Zoezi hilo la kuandikisha wapiga kura uchaguzi huo lililoanza tarehe 11 hadi 20 Oktoba mwaka huu linalenga kuandikisha wananchi 215,510.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa