Wananchiu wa Wilaya ya Magu wameshauriwa kuishi mtindo bora wa maisha unaozingatia ulaji unaofaa na kuepuka kula vyakula vyenye mafuta mengi , kuepuka matumizi ya pombe, uvutaji wa sigara , kuepuka msongo wa mawazo na kufanya mazoezi ya mwili ili kuepuka magonjwa yasioambukiza ambayo yameripotiwa kuchangia asilimia 74 ya vifo duniani kwa mujibu wa ripoti ya shirika la afya duniani ( WHO) mwaka 2022.
Wito huo umetolewa na mratibu wa magonjwa yasioambukiza Wilaya ya Magu Dokta Paulina Silvanus wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasioambukiza iliyofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Magu Jumatatu Novemba 06, 2023.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya wiki ya magonjwa yasioambukiza Dokta Paulina amesema katika vifo vyote vinavyotokea Hospitali ya Wilaya ya Magu asilimia 30 husababishwa na magonjwa yasioambukiza hivyo amesisitiza kuwa wataendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuweza kuboresha na kurekebisha mfumo na mtindo wa maisha ili kupunguza magonjwa yasioambukiza.
Amesema kuwa Hospitali ya Wilaya imeweza kuanzisha kliniki ya magonjwa yasioambukiza kama vile presha , sukari na selimundu ambayo hufanyika kila siku ya jumatano na wastani wa wagonjwa 10- 15 huudhuria kliniki hiyo.
" Pia tumeweza kufanya huduma za mikoba za utoaji elimu na upimaji wa magonjwa yasioambukiza katika kata mbalimbali ndani ya Wilaya ya Magu" amesema Dr Paulina
Kuhusu changamoto Dr. Paulina amesema kuwa uwezo duni wa kumudu ghrama za matibabu hivyo kupelekea watu wachache kuhudhuria kliniki ya magonjwa yasioambukiza.
Kwa upande wake Kiongozi wa damu salama Wilaya ya Magu Lusekelo Charles amehimiza wananchi kujitoa kwa kuchangia damu ili kuokoa maisha ya watu wengine sambamba na kujiwekea akiba pindi unapotokea uhitaji kwao binafsi.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa