Halmashauri ya Wilaya ya Magu imezindua zoezi la upandaji miti ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kuzitaka Halmashauri zote nchini kupanda miti isiyopungua Milioni moja na laki tano kila mwaka ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuhakikisha Wilaya ya Magu inafanya vizuri katika utunzaji wa mazingira.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo leo Ijumaa Novemba 17, 2023 ambayo iliamabata na zoezi la ugawaji wa miche ya miti bure , Katibu Tawala wa Wilaya ya Magu Jubilate win Lawuo amesema zoezi la upandaji miti ni faida kwa Wilaya ya Magu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya chini, kutunza mazingira , kupata vivuli na hali ya hewa nzuri , kupata mvua zenye faida katika kilimo, ufugaji na kusaidia kuinua kipato cha wananchi na Taifa kwa ujumla.
Aidha Katibu Tawala huyo amewaomba wananchi waliokabidhiwa miche ya miti kwenda kuitunza na kuhakikisha inakua ili kufikia lengo kusudiwa na si kuchukua na kwenda kuiweka nyumbani na kutoiendeleza.
Vilevile amempongeza Mhifadhi Misitu wa Wilaya ya Magu kwa kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuelekeza kila Wilaya kuwa na vitalu vya kuotesha miti na kusambaza katika maeneo mbalimbali ya Wilaya.
Kwa upande wake Mhifadhi Misitu wa Wilaya ya Magu Mashaka M. Mrisho amesema Wilaya ina bustani za kuotesha miti katika maeneo mbalimbli ili kufikia lengo la kupanda miti milioni moja na laki tano kama mkakati uliopo kitaifa kutaka kila Wilaya kufikisha idadi hiyo.
Amesema vitalu vilivyopo Wilaya ya Magu ni pamoja na kitalu cha Magu mjini ambapo wana mpango wa kuotesha miti laki tatu, Bustani ya Shule ya Msingi Nghya miti elfu 50, Busalanga Shule Msingi miche elfu 30, Shule ya sekondari Kabila miche elfu 12, bustani za watu binafsi, na vikundi kwa lengo la kuhifadhi uoto wa asili wa Wilaya ya Magu.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa