Halmashauri ya Wilaya ya Magu kupitia Idara ya viwanda biashara na uwekezaji Julai 11, 2024 wametoa mafunzo ya mifumo ya ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mfumo wa TAUSI kwa watendaji wa kata, mawiliki wa stationary na internet Cafe.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ambapo mada mbalimbali zilitolewa ikiwemo elimu ya mfumo TAUSI wa leseni za biashara na vileo, mfumo wa tausi nyumba za kulala wageni, elimu ya kodi ya majengo, vibali vya ujenzi, kodi ya mabango kutumia TAUSI na elimu ya kodi ya vibanda kwa mfumo wa TAUSI.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mohamed Ramadhani amewataka wafanyabiashara Wilayani Magu kuendelea kulipa kodi na ada mbalimbali zilizohalalishwa na Serikali kupitia mifumo ya serikali ya ulipaji na kupatiwa risiti za kieletroniki ili kuleta maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa idara ya viwanda, biashara na uwekezaji Wilaya ya Magu amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watendaji hao kuelewa mfumo wa TAUSI.
Amesema “ mafunzo haya yatakuza ongezeko la ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri yetu kwani kutokana na mlichojifunza leo naamini mtakua wasimamismizi wazuri wa mfumo wa TAUSI kwa wakusanyaji wa mapato wa Kata zenu pia ikitoke kuna changamoto yoyote linabidi mtushirikishe sisi ili tuweze kutatua tatizo hilo na kuhakikisha tunakusanya mapato kwa wingi”.
Mfumo wa TAUSI unaweza kumsaidia mwananchi kujihudumia mwenyewe pindi anapotaka kuanzisha biashara kwani ataweza kutumia simu yake ya mkononi kujisajili katika mfumo na atapata huduma zote kadiri ya anavyohitaji kwa kutumia kiunganishi(Link) ‘tausi.tamisemi.go.tz.’
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa