Maafisa Elimu Kata na Wakuu wa Shule za Wilaya ya Magu wametakiwa kutimiza wajibu wao kwa kusimamia kikamilifu suala la elimu ikiwemo kudhibiti utoro wa wanafunzi, watoto kula shuleni na kusimamia taaluma ili kuinua kiwango cha ufaulu wa Wanafunzi Shuleni.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Joshua Nassari wakati wa hafla ya kuwapongeza walimu na shule za sekondari zilizofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.
Akizungumza wakati wa halfa hiyo Dc Nassari amesema jukumu la Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa shule na Wanajamii kwa ujumla ni pamoja na kukemea tabia ya baadhi ya wanafunzi kuwa na tabia ya utoro kwakua wanafahamu vizuri maeneo wanayotoka wanafunzi wao hivyo wasimamie suala hilo kikamilifu ili kuongeza ufaulu.
Aidha aliwapongeza walimu na shule zote zilizofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa huku akitoa rai walimu hao kuendeleza wimbi la kufaulisha wanafunzi kwa mwaka huu ili kuendelea kupeperusha bendera ya Mkoa wa Mwanza kitaaluma.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mohamed Ramadhani ametaka walimu kubadilisha fikra zao na kujielekeza katika matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji wa wanafunzi pamoja na utendaji kazi wao ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Naye afisa elimu Sekondari Wilaya ya Magu Beatrice Balige amesema kuwa lengo la kutoa motisha ya pongezi kwa walimu na shule zilizofanya vizuri ni kutambua mchango na jitihada zilizofanywa na walimu ili kuongeza ushindani na kufikia lengo la kuongeza ufaulu katika shule zilizopo Wilaya ya Magu.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa