Taasisi isiyo ya kiserikali ya Sports Charity imekabidhi mipira zaidi ya 200 katika shule za msingi na Sekondari zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Magu kwaajili ya maandalizi ya michezo ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania ( UMITASHUMTA) na Mashindano Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania(UMISETA) mwaka 2024.
Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea mipira hiyo iliyofanyika leo Ijumaa machi 8, 2024 katika ukumbi wa CCM , Afisa Michezo Wilaya ya Magu Bi. Kabula Malale ameishukuru taasisi hiyo kwa kutoa mipira hiyo ambapo alibainisha kuwa itasaidia katika maandalizi ya shule za msingi na Sekondari kujiandaa na mashindano UMITASHUMTA na UMISETA.
Kuhusu maandalizi ya michuano hiyo amesema wamejipanga vizuri na zoezi la kutafuta vipaji vya wananfunzi watakaoshiriki michuano hiyo litaanza katika ngazi za kata ili kupataa wachezaji watakaoleta ushindani katika michuano hiyo.
Katika hatua nyingine Afisa Michezo huyo amewasihi wasimamizi wa michezo shuleni kuzingatia ratiba ya michezo shuleni ili kuwapa wanafunzi muda stahiki kushiriki katika michezo hali itakayopelekea kuibua na kuendeleza vipaji vyao.
Hafla ya kupokea mipira hiyo iliambatana na kikao cha tathmini ya michezo UMITASHUMTA na UMISETA ambacho kiliongozwa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo , Peter Mujaya na kuhudhuriwa na walimu wa michezo shule za msingi na Sekondari zilizopo Halmashauri ya Wilaya nya Magu.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa