Halmashauri ya Wilaya ya Magu imeishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kulitambua kundi la vijana ambao ni taifa la leo kwa kutoa fursa mbalimbali za kuinua uchumi, ajira na elimu jumuishi.
Shukrani hizo zimetolewa na Afisa tarafa ya Ndagalu, Grace Msilanga wakati wa kongamano la vijana katika tarafa hiyo kwa lengo la kuwakutanisha vijana mbalimbali wa tarafa ya Ndagalu ili kubadilishana mawazo yenye kujenga na kuleta uelewa katika nyanja za kisiasa, kiutamaduni, kiuchumi na kuhamasisha mabadiliko chanya kwa vijana kwa maendeleo endelevu.
Akizungumza katika kongamano hilo Bi Msilanga amesema serikali itaendelea kuwawezesha vijana kwa kuweka utaratibu maalum ikiwemo mafunzo ya ufundi stadi (VETA), kupandisha hadhi shule za sekondari kuwa elimu ya juu, kutoa vitambulisho kwa wafanya biashara ndogondogo ambao wengi wao ni vijana na kutoa mikopo yenye masharti nafuu.
Aidha, ametoa wito kwa vijana kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika shughuli za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa amani na utulivu na sherehe za Mwenge wa Uhuru zitakazofanyika mwezi Agosti 2025 Wilayani Magu.
Kwa upande wake Afisa maendeleo ya Vijana Wilaya ya Magu Bi. Prisca Salum amesema kongamano hilo limebeba ujumbe wa mbio za mwenge wa uhuru 2025 unaosema “JITOKEZE KUSHIRIKI UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2025 KWA AMANI NA UTULIVU” ambapo kauli mbiu hii inamaanisha vijana kujitambua , kujitokeza kugombea, kushiriki kupiga kura kwa kuchagua viongozi bora.
Amesema vijana wamejengewa uwezo wa kuipenda nchi yao na kudumisha utamaduni wenye maadili na mahusiano mema baina yao.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa