MKUU wa Wilaya ya Magu, Joshua Nassari leo Jumatatu amewaongoza watumishi wa Halmashauri ya wilaya hiyo pamoja na wanafunzi wa shule ya sekondari Magu kupanda miti katika hospitali ya wilaya ya Magu katika kusherehekea siku ya kuzaliwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais Samia ambaye ametimiza umri wa miaka 65, ni mmoja wa viongozi wanaohamasisha wananchi kutunza mazingira kwa kutumia nishati safi ya kupikia badala ya kukata miti kwa ajili ya matumizi ya kuni.
Akizungumza katika hafla hiyo ya upandaji miti, DC Nassari ambaye pia alikuwa ameambatana na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mohamed Ramadhani, amesema miti hiyo ya matunda inalenga kuwaelimisha wananchi watakaofika kupata huduma hospitalini hapo kuhusu umuhimu wa kula matunda.
“Mama mjamzito anapofika kupata huduma katika eneo hili, daktari anapomsisitiza kula matunda ili kumpa afya hata mtoto aliye tumboni, pia anaweza kutoka nje na kumuonesha matunda hayo, ndio maana hapa tumepanda miti ya matunda pekee,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa wilaya hiyo amewataka wanafunzi waliohudhuria hafla hiyo kwenda kuotesha miti ya matunda katika makazi yao na kuhakikisha miti hiyo inastawi.
“Mimi nitajitolea kuhakikisha mnapata miti hii ya matunda mbalimbali kwa wakala wa misitu (TFS) au hapa halmashauri. Lengo letu ni kwenda sambamba na malengo ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan ambaye anahamasisha wananchi kupanda miti ili kulinda mazingira yetu.
“Miti ina faida nyingi kwa sababu inatoa hewa ya oxygen ambaye tunaivuta, nayo inavuta hewa ya carbondioxide ambayo sisi tunaitoa, lakini mbali na kivuli inatupatika matunda yanayoimarisha kinga na kutupatia virutubisho mbalimbali katika miili yetu,” amesema.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa