Mkuu wa Wilaya ya Magu Mwl. Khadija Nyembo amehutubia Wananchi katika kilele cha Maadhimisho ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika Wilaya ya Magu kata ya Kitongosima Kijiji cha Lugeye. Ameanza kwa kuwashukuru viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu na wananchi wote kwa ujumla kwa heshima kubwa ya kuwa mgeni rasmi. Aidha, ameupongeza uongozi wote wa Kata ya Kitongosima hasa Mheshimiwa Diwani na viongozi wa Vijiji vya lugeye, Kigangama na Kitongosima kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuandaa sherehe.
Amesema Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Maendeleo Endelevu 2030, Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa Watoto”. Ni jukumu la serikali na jamii yetu kwa ujumla, kuona kuwa ulinzi wa mtoto unaimarishwa kuanzia ngazi ya kaya na jamii kwa ujumla, aidha Serikali ihakikishe watoto hasa wa kike wanapata haki za kuishi, kuendelezwa, kulindwa, kushiriki na kutobaguliwa katika masuala mbali mbali ya Kijamii na Kiserikali. Watoto wengi hasa wenye ulemavu wanakabiliwa na matatizo mbalimbali, ambao ni jukumu letu kuwatetea na kuwalinda.
Jukumu la kulea, kutunza na kuwaendeleza watoto ni letu sote, Kila mmoja wetu anao wajibu wakuhakikisha kwamba watoto wanakua na kuishi katika mazingira yaliyo bora na salama. Hata hivyo wajibu wa kwanza upo mikononi mwa wazazi yaani Baba, Mama na walezi. Hawa ndiyo nguzo muhimu ya maisha ya watoto wetu, aidha wanao wajibu mkubwa wa kuhakikisha watoto wanapata mahitaji yao yamsingi ikiwani pamoja na mapenzi ya wazazi ili kuwawezesha kukua katika hali ya upendo na furaha.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa