Katibu Tawala (W) Ndg. F. Nyoni alimwakilisha Mkuu wa Wilaya katika maadhimisho ya kilele cha wiki ya maji Duniani yaliyofanyika Ki-wilaya Katika kata ya Ng’haya. Ameanza kwa kufungua kisima kirefu cha maji katika kijiji cha Ng’haya ambapo amewapongeza wananchi na wageni waalikwa kwa kuhudhuria maadhimisho hayo, kwani ni muhimu katika kufanya tathimini ya maji ambayo ni changamoto kubwa inayokabili Wilaya ya magu. Amesisitiza Jamii ya watumiaji maji na wananchi kwa ujumla kutunza miundombinu ya maji chini ya usimamizi wa Viongozi ngazi ya Kijiji hadi ngazi ya Wilaya. Ameeleza kuwa, Mkandarasi ameanza kazi ya kutekeleza Mradi mkubwa wa maji Bomba Magu Mjini ambapo yote hayo ni juhudi za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata maji ya kutosha. Amewaasa wananchi kushirikiana na viongozi katika kutunza vyanzo vyote vya maji pamoja na kupanda miti ili kukabiliana na changamoto ya maji. Kwa kuwa maeneo yetu wakati mwingine hayapati mvua za kutosha, ameshauri wananchi kupanda mazao yanayostahimili ukame kama vile Mtama, Mihogo, na Viazi kwa sababu ya changamoto za ukame katika wilaya yetu.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa