Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Mwaka, 2019 Ndugu, Mzee Mkongea Ali amevutiwa na mshikamano wa viongozi wa Serikali Wilayani Magu na amewataka watalaam na watendaji wa Serikali Wilayani Magu kuendelea na umoja huo katika kusimamia miradi ya maendeleo kwa weledi kwa mujibu wa taaluma zao, haya yamejili katika mbio za mwenge wa Uhuru Wilayani Magu tarehe 20.05.2019.
Akitoa ujumbe wa mbio za mwenge, Kiongozi wa mbio za mwenge amepongeza viongozi wa Wilaya ya Magu kwa mshikamano na ushirikiano uliopo Wilayani wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya Dr. Philemon Sengati (PhD), Mkurugenzi Mtendaji Wilaya Lutengamo G. Mwalwiba, Mheshimiwa Mbunge wa jimbo la Magu Destery B. Kiswaga pamoja na Viongozi wa chama cha Mapinduzi.
Aidha amewataka wananchi kufanya kazi kwa bidii, kudumisha umoja na mshikamano na kulipa kodi. Katika kaulimbiu isemayo “Maji ni haki ya kila mtu, Tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa” amesema “ Serikali inafanya juhudi za kuondoa kero ya maji kwa wananchi wake na kuwapatia maji safi na salama. Katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, chagua viongozi bora, waadilifu na wachapa kazi. Wananchi wajitokeze kupima Afya zao kwa hiari ili kuepuka maabukizi mapya ya VVU, kuacha kutumia dawa za kulevya, kuepuka malaria kwa kutumia chandarua kwa usahihi na kupinga Rushwa”
Amekabidhi hundi zenye jumla ya Tshs 46,000,000.00 kwa vikundi 13 vya wanawake, vikundi 3 vya vijana na vikundi 2 vya watu wenye ulemavu na amesema miradi yote imepita bila kupingwa.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Magu Dr. Philemon Sengati ametoa taarifa fupi mbele ya kiongozi wa Mwenge Kitaifa kuwa Mwenge utachochea maendeleo katika Wilaya ya Magu kwa kutembelea miradi 11, ambayo itafunguliwa, kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi. Na Kwamba Dr. Sengati amesisitiza kuwa Wilaya ya Magu ni bora katika Mkoa wa Mwanza kwenye suala la maendeleo.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa