Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Godfrey Mzava ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya Nyanguge wilayani Magu mkoani Mwanza na kueleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo.
Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa uhuru ameweka jiwe hilo la msingi mwishoni mwa wiki baada ya kukagua mradi huo na kuridhishwa na ujenzi wake ambao ulianza tarehe 25 Februari mwaka 2022.
Awali Mratibu wa Mwenge wa uhuru Wilaya ya Magu, Peter Mujaya, alisema utekelezaji wa mradi huo hadi kukamilika Juni 2024/2025, unakadiriwa kutumia jumla ya Sh milioni 250, fedha kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri.
“Mpaka sasa Halmashauri imeshatoa jumla ya Sh milioni 150 kati ya fedha hizo kiasi cha Sh milioni 123 kimetumika kununua vifaa vya ujenzi na kulipa mafundi ujenzi. Mpaka sasa ujenzi upo katika hatua ya ukamilishaji, amesema.
Akizungumzia mradi huo, Mzava aliipongeza halmashauri hiyo kwa kuwekeza nguvu katika kuboresha huduma ya mama na mtoto hasa ikizingatiwa ni makundi ambayo yana uhitaji mkubwa wa afya bora kwa kizazi cha baadae.
Aidha, akizungumzia mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria katika wilaya ya Magu, Mzava aliipongeza halmashauri hiyo kwa kufanikiwa kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo kutoka asilimia 18.9 mwaka 2023 hadi asilimia 12.7 mwaka 2024.
Pamoja na jitihada hizo alitoa wito kwa jamii kuhakikisha wanatumia dozi za malaria ipasavyo bila kukatisha na kutumia dawa za kienyeji ili kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa uhuru pia alitoa wito kwa wilaya hiyo kuendelea kutoa elimu Pamoja na kudhibiti maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) ili kulinda afya za wananchi wa wilaya hiyo.
Pia aliipongeza wilaya ya Magu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa masuala ya lishe kuendelea kusimamia kikamilifu suala la lishe bora kwa wananchi wote kwa kuhakikisha kuwa inapunguza tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Alitoa wito kwa jamii kuzingatia umuhimu wa unyonyeshaji maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo ili kuwa na jamii yenye afya imara katika kutekeleza shughuli za kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stagomena Tax alisema ujenzi wa wodi hiyo ya wazazi ni muendelezo wa hlamshauri hiyo kuboresha huduma za afya.
“Hakuna maendeleo bila afya, hivyo natoa wito kwa wananchi wenzangu kutunza miundombinu ya mradi huu kwa sababu mbali na huduma za afya itatufungulia pia milango ya kiuchumi,’ alisema.
Pamoja na mambo mengine alitoa wito kwa wananchi kwenda kujiandikisha katika daftari la uchaguzi wa serikali za mitaa lililofunguliwa tarehe 11 Oktoba mwaka huu hadi tarehe 20 Oktoba ili kumchagua kiongozi atakayeungana na serikali kuwaletea maendeleo.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa