Mkuu wa Wilaya Magu Mhe. Khadija Nyembo azungumza na wadau wa elimu katika kikao kilichofanyika terehe 30.03.2017 katika ukumbi wa Magu Sekondari. Wakati akifungua kikao hicho ameeleza kuwa lengo kuu la kuitisha kikao hicho cha wadau wa elimu ni kuona hali halisi ya elimu katika wilaya ya Magu, changamoto zinazokabili elimu na kujadili mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto zilizopo ili kuleta ufanisi wa elimu katika wilaya ya magu.
Katika kujadili changamoto na mikakati, wadau wameshauri kamati za maendeleo ya kata kutenga maeneo ya kujenga shule mpya ili shule zenye wanafunzi wengi zaidi ya 1260 zigawanywe. Kwa kufanya hivyo kutakuwepo na ufanisi katika suala zima la ufundishaji na ufaulu wa wanafunzi utaongezeka. Wadau hao wamesisitiza walimu kuwa na nia ya ufundishaji na uwajibikaji katika shule zao, kwa walimu wasiotimiza wajibu wao wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Aidha wadau hao wamepongeza Shule ya Mugini kwa kufanya vizuri kiwilaya, Mkoa na Kitaifa katika Matokeo ya mtihani wa mwisho. Walishauri serikali ijali kada ya ualimu ili watu wabadili mtazamo uliopo kuwa walimu ni “Wito” kwani Kazi ya ualimu inaonekana ni chaguo la mwisho baada ya kukosa vyuo vinavyotoa taaluma nyigine. Miundombinu itakayowezesha wanafunzi kujifunza vizuri iboreshwe na walimu wote wakumbushwe maadili ya ualimu ili waweze kusimamia taaluma vizuri.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa