HATIMAYE Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhani amefungua rasmi utoaji huduma katika shule mpya ya sekondari Bundilya iliyopo katika Kijiji cha Bundilya kata ya Kahangara wilayani humo.
Shule hiyo iliyojengwa kwa gharama ya Sh milioni 584.2 fedha za Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP), ujenzi wake ulianza Septemba mwaka jana na kukamilika Juni 30, mwaka huu.
Akizungumza na wananchi pamoja na baadhi ya wanafunzi waliohudhuria hafla ya ufunguzi huo wa utoaji wa huduma shuleni hapo, Mkurugenzi huyo amewapongeza wananchi wa Kijiji hicho cha Bundilya kutokana na nguvu kazi waliyoitoa hadi kufanikisha ujenzi wake.
“Mwaka jana tulikuwa pamoja hapa na viongozi wote tukachimba msingi pamoja. Wananchi walichangia mchanga tripu 90 sio ndogo! pia walichangia maji tangu ujenzi unaanza. Ushirikiano huu maeneo mengine hatuupati hivyo tunawashukuru sana,” amesema.
Pamoja na mambo mengine ameiasa jamii kushirikiana kuhakikisha watoto wao wanasoma ikiwamo kuweka utaratibu maalumu wa uchangiaji wa chakula na kuhakikisha kunakuwepo an mazingira rafiki ya watoto kusoma.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi wa shule hiyo, Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Kahangara, James Ndega amesema lengo la mradi huo kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya sekondari kwa kuwapunguzia umbali wanafunzi na kupunguza msongamano katika shule ya sekondari Kahangara na kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora wawapo shuleni.
“Mradi unaenda kupokea wanafunzi 79 wa kidato cha kwanza kutoka shule mama ya Kahangara sekondari, miongoni mwao 35 ni wasichana na 44 ni wavulana. Mradi ulitengeneza ajira 57.
“Pia imejengwa miundombinu 11 inayojumuisha madarasa manne na ofisi mbili, jengo la maabara ya fizikia, baiolojia, kemia, jengo la utawala, maktaba, kompyuta na vyoo matundu nane ambapo manne ya wavulana na manne wasichana pamoja na tanki la maji kuvuna maji ya mvua,” amesema.
Naye Afisa Elimu Sekondari Magu, Beatrice Balige amesema kukamilika kwa shule hiyo kumeongeza idadi ya shule katika wilaya ya Magu kufikia 42 za Sekondari.
“Shule tayatri imepata usajili tarehe 3 Julai mwaka huu kwa namba 7008. Tunashukuru kwa ushirikiano mkubwa tuliopata kutoka kwa wananchi na mafundi waliofanya kazi hii kwa uweledi mkubwa.
“Sasa tumewapokea wanafunzi tusipowapa maarifa ya kutosha jitihada hizi zitakuwa zimepotea. Tunahitaji mzazi ufanye sehemu yako na jamii vivyo hivyo. Wazazi tuna wajibu wa kuhakikisha wanafunzi wetu wanaenda kwa mienendo mizuri ili kufikia malengo yao,” amesema.
Aidha, baadhi ya wazazi wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa shule hiyo hasa ikizingatiwa inakwenda kupunguza changamoto ya watoto kutembea umbali mrefu kufuata huduma katika shule ya sekondari Kahangara.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa