KAMATI ya Ushauri ya Wilaya ya Magu (DCC) imepitia na kujadili mapendekezo ya rasimu ya mpango na bajeti ya halmashauri kwa mwaka 2025/2026 ambayo imependekeza kuidhinishwa jumla ya Sh. 64.2 bilioni kutoka vyanzo mbalimbali na kutoka ruzuku ya Serikali Kuu.
Akiwasilisha rasimu ya bajeti hiyo leo Alhamisi mbele ya Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Magu, Joshua Nassari, Afisa Mipango wa wilaya, Pastory Mukaruka amesema bajeti hiyo inalenga kuzingatia vipaumbele vinne.
Mukaruka ambaye aliwasilisha rasimu hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhani, ametaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuimarisha utawala bora unaohusisha kusikiliza, kupokea na kushughulikia kero za wananchi na ulipaji wa fidia ya ardhi kwa wananchi waliotwaliwa maeneo yao kwa ajili ya shughuli za umma.
Kipaumbele cha pili ni kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa makundi yote, kuboresha hali ya Lishe na ukamilishaji wa miundombinu ya afya, kuendeleza ujenzi wa Kituo cha Afya Nyanguge, kukamilisha ujenzi wa zahanati 6, kituo 1 cha Afya na nyumba 2 za Watumishi wa kada ya Afya na kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji shuleni.
“Tatu ni kuimarisha na kuongeza wigi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuongeza ubora na utoaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kutoka bilioni 4.73 mwaka 2024/2025 hadi kufikia bilioni 5.23 ifikapo mwaka 2026.
“Kuendeleza ujenzi wa stendi ya kisasa ya Wilaya eneo la Ilungu na stendi ya magari madogo (Hiance) kona ya Kayenze, kujenga ukumbi wa mikutano wa Halmashauri, kupandisha hadhi mnada wa Nyanguge kuwa mnada wa upili,” amesema.
Kipaumbele cha mwisho amesema ni kuiwezesha jamii katika uboreshaji wa masuala ya jinsia na ustawi wa jamii, kuinua uchumi wa makundi maalumu, kuwezesha kutoa mikopo wa 10% kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Aidha, amezema katika kipindi cha mwaka 2024/2025 Halmashauri ilipanga kukusanya na kutumia jumla ya Sh bilioni 56.9 kutekeleza Shughuli mbalimbali za maendeleo na matumizi ya kawaida.
Awali akifungua kikao hicho, DC Nassari amesema lengo kushirikisha wadau wote muhimu wa halmashauri hiyo kushiriki kikamilifu katika upangaji na kupata ufafanuzi wa mapato na matumizi ya wilaya hiyo.
Pamoja na mambo mengine amesema katika bajeti inayoishia mwaka huu wa fedha 2024/2025, halmashauri hiyo imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwamo kuboresha makusanyo hadi kutoka asilimia 57 hadi kufikia asilimia 97.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa