Wizara ya Katiba na Sheria imetoa mafunzo ya utawala bora na uraia kwa kamati ya usalama ya wilaya ya Magu, wakuu wa idara mbalimbali za halmashauri na watendaji wa kata wilaya hiyo ili kuwakumbusha kuzingatia mipaka katika utumishi na misingi ya utawala bora pamoja na kukuza utaifa na uzalendo miongoni mwao.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo jana Jumatatu wilayani Magu mkoani Mwanza, Wakili wa serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ambaye pia ni mratibu wa mafunzo hayo, Dorice Dario amesema mafunzo hayo ni kuendeleza mkakati wa serikali katika kuwawezesha watumishi umma katika kada zote kutekeleza ipasavyo falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu 4R.
Pia amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha na kuwajengea uwezo washiriki ili waelewe namna ya kutekeleza majukumu yao kwa kufuata misingi ya utawala bora na haki za binadamu na demokrasia.
"Mafunzo haya ni utekelezaji wa falsafa ya Rais Samia ya ‘Rebuilding’ (kujenga upya) ambapo tunaamini tukimaliza mafunzo haya washiriki wote watakuwa wamejengwa upya uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha kwa wananchi,” amesema.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mohamed Ramadhani amesema dhana ya mafunzo hayo ni kuimarisha utoaji bora wa huduma kwa wananchi.
“Tunatarajia matokeo ya mafunzo haya tuyaone kwa wananchi. Hivyo, tukae tupokee tukayatekeleze ili amani iendelee kutawala kwa wananchi,” amesema.
Akizungumza baada ya kupata mafunzo hayo, Afisa Mtendaji wa kata ya Nkungulu, Sara Kunzugala mbali na kuishukuru Serikali kwa kuwapatia mafunzo hayo, amesema mafunzo hayo yatasaidia kuwa chachu ya mabadiliko katika vituo vya kazi hasa ikizingatiwa wao wanajumuika moja kwa moja na wananchi katika kutekeleza majukumu yao.
“Tumejengewa uwezo wa kuwaelewesha wananchi namna ya kutambua haki zao, kwa hiyo tutatumia mafunzo haya kuwaambia wananchi wasiwe na hofu kudai haki zao na tutawaelekeza njia sahihi za kutekeleza lengo hilo,” amesema.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa