Kamati ya fedha, uongozi na mipango katika halmashauri ya wilaya ya Magu imeeleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo.
Hayo yamebainishwa katika ziara ya kamati hiyo iliyofanyika leo tarehe 16 Januari 2025 na kuongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mpandalume Simon pamoja na watalaam mbalimbali wa Halmashauri ya wilaya ya Magu.
Katika ziara hiyo, kamati ilikagua ukamilishaji wa jengo la Mama na mtoto, wodi ya wanaume na Bohari ya dawa mradi uliotumia kiasi cha Sh milioni 40.
Pia ilikagua ujenzi wa stendi ya Ilungu ambao kwa awamu ya kwanza imetumia sh milioni 130 na unatarajiwa kukamilika baada ya miezi mitatu, ukamilishaji wa nyumba vinne vya madarasa katika shule ya sekondari ya Nyashimba uliogharimu Sh milioni 50 na vyumba viwili vya maabara katika shule ya sekondari Nyamahanga uliogharimu Sh milioni 50.
Akizungumzia kuhusu ukamilishaji wa jengo la Mama na mtoto, wodi ya wanaume na Bohari ya dawa mradi, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Magu, Dk. Mhana Raphael amesema awamu ya kwanza walipokea milioni 700 kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo ambapo ulitekelezwa 2022 hadi 2023 na fedha ilipoisha mradi ukasimama.
Amesema sasa fedha zilizotolewa na halmashauri zimekamilisha ujenzi huo na sasa majengo yameanza kutumika.
Aidha alisema awamu ya pili anatamani serikali iweke mkazo katika ujenzi wa wodi ya watoto, wodi binafsi na jengo la dharura.
Kwa upande wa majengo ya madarasa, mwenyekiti wa halmashauri alisema anatarajia kuanzia Februari mwaka huu, wanafunzi wataanza masomo katika shule hizo baada ya halmashauri kuridhia kutoa kiasi cha Sh milioni 20 kwa kukamilisha ujenzi wa madarasa hayo.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa