Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele leo Jumatano Aprili 23, 2025 amekutana na wadau wa uchaguzi katika jimbo la Magu kwa lengo la kujadili na kupitia mapendekezo ya ombi la kugawa jimbo hilo.
Hatua hiyo imekuja baada ya wadau hao kuridhia jimbo hilo ligawanywe majimbo mawili ambayo yataitwa Magu na Sanjo.
Akifungua kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi za mkuu wa wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Jaji Mwambegele amesema lengo la kikao ni kujiridhisha na takwimu na jina la jimbo kama maombi yalivyowasilishwa ikiwa ni sehemu ya jukumu la tume la kuwashirikisha wadau wake wa uchaguzi.
Amesema kupitia kikao hicho tume itajiridhisha kuhusu taarifa mbalimbali zilizopo kwenye maombi ya kugawa jimbo la Magu yaliyowasilishwa tume ya uchaguzi.
Ameongeza kuwa taarifa ambazo tume itapenda kujiridhisha ni pamoja na mgawanyo wa kata, mipaka iliyopendekezwa, ramani ya jimbo linalopendekezwa kugawanywa na idadi ya watu kama amabavyo imependekezwa pamoja na jina la jimbo lililowasilishwa tume.
Akichangia mapendekezo hayo, Mbunge wa jimbo hilo, Boniventura Kiswaga (CCM), ameunga mkono mapendekezo hayo yaliyowasilishwa INEC na kueleza kuwa kutakuwa na faida nyingi iwapo pendekezo hilo litaridhiwa.
Naye Diwani wa Kata ya Bukandwe, Marco Minzi (CCM) amesema ugawaji wa jimbo hilo utarahisisha uletaji wa maendeleo kwa wananchi tofauti na sasa ambapo jimbo lina kata 25.
Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi wa ngazi ya mkoa na Wilaya na wadau wa uchaguzi jimbo la Magu ambao kwa pamoja katika kikao hicho wamekubaliana na taarifa zilizowasilishwa kuomba kugawanywa kwa jimbo hilo.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa