TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeeleza kuridhishwa na zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura katika jimbo la Magu kutokana na kasi ya maboresho pamoja na muitikio mkubwa wa wananchi katika zoezi hilo linalofanyika kwa siku saba.
Hayo yamebainishwa leo Jumamosi tarehe 3 Mei, 2025 na Mjumbe wa tume hiyo, Dk. Zakia Mohamed Abubakar ambaye ametembelea kata mbili za halmashauri ya wilaya Magu.
Akiongozwa na Afisa Mwandikishaji Jimbo la Magu, Mohamed Ramadhani, Dk. Zakia amepongeza hamasa iliyotolewa katika jimbo hilo hali iliyowezesha wananchi kujitokeza kwa wingi kuhakiki majina yao katika daftari la awali, kukata kitambulisho cha mpiga kura kwa wale ambao hawakupata fursa awali, waliopoteza, kuharibika au kufikisha umri wa miaka 18.
Dk. Zakia akiwa ameambatana na maofisa uchaguzi, ametembelea vituo vya Shule ya Msingi Kanyama na Ofisi ya Mtendaji wa Kata Bujora vilivyopo katika kata ya Bujora pamoja na kituo cha Ofisi ya mtendaji kata ya Kisesa kilichopo kata ya Kisesa.
Zoezi hilo la maboresho ya daftari la kudumu la wapiga kura kwa awamu ya pili katika jimbo la Magu linafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 1 hadi 7 Mei mwaka huu.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa