Halmashauri ya Wilaya ya Magu imetembelewa na wageni kutoka Benki ya Dunia, Ikulu, TASAF Makao Makuu na TASAF Mkoa. Lengo la ugeni huo ni kuangalia dhumuni la Malipo yanavyofanyika kwa walengwa wa kaya Maskini katika Mamlaka za Serikali za mitaa sambamba na maandalizi ambayo serikali imeanza kufanya kwa ajili ya kunusuru kaya maskini awamu inayofuata. Halmashauri ya Wilaya ya Magu ni Miongoni mwa Halmashauri nne (4) zilizotembelewa kwa niaba ya Halmashauri zote 185 Tanzania Bara kwani imeonekana kufanya vizuri katika kutekeleza shughuli za kunusuru kaya Maskini. Ziara hiyo pia imefanya Mapitio ya kawaida ya utekelezaji ya nusu mwaka.
Wageni hao wamepokea mapendekezo mbalimbali ya kuboresha huduma za TASAF kutoka kwa wakuu wa Idara za Halmashauri na vitengo. Wakuu hao wa Idara wameanza kwa kupongeza kazi nzuri zinzofanywa na TASAF kwani katika idara ya Afya mahudhurio ya klinik yameongezeka, Lishe na wananchi wengi wamejiuga na CHF kupitia mradi wa TASAF. Wanafunzi wanaohudhuria shuleni wameongezeka na wanafika shuleni kwa wakati kwa sababu wanatimiziwa mahitaji yao. Wakuu wa idara wameshauri kuangalia dhana ya uendelevu kwa walengwa ili waweze kutoka hatua moja kwenda nyingine.
Wameshauri kuweka Mpango mzuri na usimamizi ili matokeo yaonekane kwa walengwa, kusaidia walengwa kwa vikundi ambapo wao wenyewe wataibua kitu cha kufanya ili wawezeshwe, kubainisha kundi la watoto yatima ili waweze kusaidiwa, kuangalia maeneo mengi yenye umasikini kama vile Wavuvi na wasaidiwe kujikinga na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI, kuweka kipaumbele cha maji kwenye mradi ujao na miundombinu mbalimbali itakayowasaidia walengwa na kuweka uhusiano mzuri kati ya TASAF na Halmashauri.
Mkurugezi Mtendaji (W) amewashukuru wageni kutoka TASAF kutembelea wilaya ya Magu. Aidha wageni pia wameshukuru kwa ushirikiano uliooneshwa na Uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Magu nakupongeza kusimamia vizuri mradi wa Kunusuru kaya Maskini.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa