WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax ametoa msaada wa mashine mbili za kudurufu mitihani kwa shule ya msingi Moha na shule ya sekondari Magu mjini zilizopo wilaya Magu mkoani Mwanza.
Pia Dk. Tax ametoa msaada wa madawati 75 katika shule ya msingi Nyalikungu iliyopo wilayani humo ambayo ni shule aliyohitimu elimu ya msingi.
Dk. Tax ambaye alikuwa ameambatana na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhani, ametoa misaada hiyo leo Jumamosi tarehe 5 Julai, 2025 na kupokewa na wakuu wa shule hizo, walimu, madiwani, wazazi pamoja na wanafunzi.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Dk. Tax amesema amewiwa kutoa msaada huo baada ya walimu na viongozi wa shule hizo kumfuata kumuomba awasaidie kutatua changamoto hizo ambazo kubwa ni mashine ya kudurufu mitihani lakini pia kumaliza tatizo la wanafunzi kukaa chini.
Pamoja na mambo mengine ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Magu kwa kufanya kazi kubwa kwa kuboresha sekta ya elimu wilayani humo ikiwemo kujenga shule mpya, kuongeza matundu ya vyoo pamoja na madawati.
“Nakumbuka mlinifuata kwa muda kidogo kuhusu photocopy, kwa kuwa ninaowajibu pia ya kuwatumikia wananchi sasa nimewaletea, ninawaomba muitumie vizuri,” amesema.
Aiddha, ameto wito wakazi wa Magu na watanzania kwa ujumla kuwa wakati Taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu, wanatakiwa kuchagua viongozi sahihi kwa maendeleo ya Taifa.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mohamed Ramadhan naye amemshukuru waziri huyo wa ulinzi kwa uzalendo wake kwani uwepo wake umekuwa ni fursa kipekee kwa wananchi wa Magu hasa kwa kuwasaidia kupata vitu mbalimbali.
Pamoja na mambo mengine ameahidi kuendelea kushughulikia changamoto mbalimbali za shule hizo ikiwemo kuongeza samani za ofisi za walimu kwa shule ya msingi Nyalikungu na kuhakikisha umeme unafika katika shule ya msingi Moha.
Akitoa shukrani kwa kupokea madawati hayo, Mwalimu mkuu msaidizi wa Nyalikungu, Alestidia Kokuijuka amesema sasa tatizo la wananchi kukaa chini au kuja kwa zamu shuleni hapo limekwisha.
“Tumepokea madawati 75, tunashukuru mheshimiwa waziri kwa sababu watoto walikuwa wanakaa chini, ila walikuwa wanakuja asubuhi na wengine mchana. Mara ya kwanza ulituletea madawati 100 yakasaidia kuondoa tatizo la wanafunzi kuja kwa zamu sasa wanafunzi wote wanaweza kukaa kwenye madawati,” amesema.
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Haki zote zimehifadhiwa